WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), baada ya kufuta uteuzi wa wajumbe wote wa bodi ya kuanzia Novemba 6 mwaka huu na kuteua wengine wapya wanane wanaounda bodi hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa kwa umma na Wizara ya Uchukuzi, inaeleza kuwa Waziri Dk Mwakyembe amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 6 (2) cha Sheria ya Bandari na kifungu cha 1(2)(i) cha jedwali la kwanza la sheria hiyo. Waliofutwa ujumbe wa bodi ni pamoja na Dunstan Mrutu, Mhandisi George Ally na Mtutura Mtutura. Wengine ni Emmanuel Mallya, Mwantumu Malale na Maria Kejo.
Walioteuliwa kuingia kwenye bodi hiyo ni Dk Jabiri Kuwe Bakari, John Ulanga, Cariline Temu na Jaffer Machano. Wengine ni Hildebrand Shayo, Said Salum Sauko, Mhandisi Julius Mamiro na Asha Nassoro. Taarifa hiyo inasisitiza kuwa mabadiliko haya ni sehemu tu ya hatua ambazo wizara inachukua kurejesha ufanisi katika mamlaka hiyo ili iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Mwakyembe ameendelea kufanya mabadiliko katika safu ya TPA ambapo alianza kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe, manaibu wake pamoja na mameneja wengine. Tangu Dk Mwakyembe achukue Wizara ya Uchukuzi amekuwa akisafisha sekta za wizara hiyo ambapo awali alianzia katika Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kwa kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Paul Chizi pamoja na watumishi wengine wanne. Nafasi ya Chizi alipewa Kepteni Lusajo Lazaro ili aendelee kuiongoza kampuni hiyo kuanzia Juni 5 mwaka huu.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz