DK. Mukangara ataka halmashauri kutenga bajeti ya michezo

WAZIRI wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara amezitaka halimashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatenga bajeti kutosha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya michezo.
Aidha , amewataka wazazi na walezi kuwahimiza vijana kupenda michezo.
Kauli hiyo ilitolewa na na Dk. Mukangara leo (jana) wakati akifungua mashindani ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanayoendelea katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.
Mashindano hayo,ambayo yamehudhuriliwa na wadau mbalimbali wa sekta ya michezo wakiwemo baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Michezo ni ajira ninaziagiza Halimashauri zote kufanya yafuatayo kutenga bajeti ya michezo ya kutosha, kuajiri maafisa michezo, kuwaendeleza walimu wa michezo, kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa na kiwanja cha michezo kilichobora na kuhamasisha wanafunzi wa kike kucheza mpira wa miguu,” alisema Dk. Mukangara huku akisisitiza kuwa hatuna budi kuwekeza katika michezo kwa gharama yoyote.
Aidha Dk. Mukangara aliwataka wadau hao kujipanga ili kuhakikisha wanatoa wanamichezo wa riadhaa kutoka mashuleni. Pia aliwataka wadau hao, kuwa na utaratibu wa kushindanisha michezo hiyo na shule za jirani.
Dk. Mukangara aliwataka wanafunzi hao kucheza kwa nidhamu na kuheshimu muda wa kucheza na kusisitiza kuwa michezo inadumisha umoja wa kitaifa hivyo aliwaaasa kuendeleza urafiki.
Naye Naibu Waziri wa TAMISEMI, Kassium Majaliwa alisema serikali kupitia wizara hizo inaendelea kufanya jitihada za kutosha za kuibua vipaji mbalimbali ya michezo kwa ajili ya timu ya Taifa. Hivyo michezo hiyo itakuwa inachezwa katika kipindi cha likizo ili kutoa muda wa masomo na michezo.
Waziri Majaliwa aliongeza mchakato wa unaendelea wa kuajiri maofisa michezo, vijana na utamaduni.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI Jumanne Sagini alizitaka halimashauri zinazopima viwanja katika maeneo ya shule kuacha tabia hiyo, badala yake zitafute maeneo mengine ya kupima.
Michezo hiyo inatarajiwa kumalizika Juni 29, mwaka huu na imeshirikisha wanafunzi 1664 kutoka kanda 12 za Tanzania ikiwemo ya Kanda ya Zanzibar.
Michezo unayoshindanishwa ni Soka, mpira wa kikapu, wavu, netibali, meza mikono na bao.
Ufunguzi wa mashindano hayo ulianza kwa mchezo wa soka ya wanawake kati ya Kanda ya Mashariki na Kusini ambapo ahadi mwandishi wa habari hizi anaondoka uwajani hapo Kanda ya Mashariki ilikuwa imefunga bao 2 na Kusini moja.