Dk. Msonde Apewa NECTA Rasmi, JK Awaapisha Majaji Wapya Dar

Dk. Charles Msonde kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA)..

Dk. Charles Msonde kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA)..

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemteua Dk. Charles Msonde kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA). Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam Agosti 14, 2014, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa uteuzi huo ulianza, Agosti 13, 2014. Kabla ya uteuzi wake, Dk. Msonde alikuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo hilo la mitihani.

Dk. Msonde anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Joyce Ndalichako, ambaye amerudi kuendelea na kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kumaliza likizo yake ya kujinoa (Sabbatical Leave).

Wakati huo huo; Rais Kikwete amewaapisha majaji 20 wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao aliwateua mwanzoni mwa wiki. Halfa hiyo iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman, Waziri wa Katiba na Sheria, Asha Rose Migiro na Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu.

Majaji hao wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni pamoja na akinamana wanane na uteuzi huo wa Rais Kikwete umeshirikisha wanasheria kutoka Serikalini, Taasisi za Umma, Jumuia ya Afrika Mashariki, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia.
Majaji hao wapya ambao wameapishwa leo ni Jaji Penterine Muliisa Kente, Jaji Benedict Batholomew Mwingwa, Jaji Eliezer Mbuki Feleshi, Jaji John Eudes Ruhangisa, Jaji Winfrida Beatrice Korosso, Jaji Lilian Leonard Mashaka, Jaji David Eliad Mrango, Jaji Edson James Mkasimongwa, Jaji Mohamed Rashid Gwae na Jaji Firmin Nyanda Matogoro.

Wengine ni Jaji Leila Edith Mgonya, Jaji Barke Mbaraka Abdou Sehel, Jaji Awadhi Mohamed, Jaji Lugano J. Mwandambo, Jaji Rose Ally Ibrahim, Jaji Paul Kihwelu, Jaji Modesta Opiyo Makopolo, Jaji Amour Said Khamisi, Jaji Mary Caroline Levira na Jaji Salma Maghimbi.