Na Magreth Kinabo– MAELEZO
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda anatarajiwa kuzindua Maonesho ya Sita ya Wazi kwa kutumia vifaa vya sauti na picha vyenye ubora wa hali ya juu vya Sony Corporation ili kutoa elimu na burudani katika kupambana na maambukizi wa virusi vya Ukimwi.
Hayo yameelezwa leo na Dk. Amos Nyirenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano ulioshirikisha Shirika lisilo la kiserikali la AMREF Tanzania. Sony Corporation na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) uliofanyika kwenye hoteli ya Holiday Inn –Jijini Dar es Salaam.
“Tutatumia mitambo ya teknolojia ya habari ya hali ya juu kutoka Sony ili ambapo tutatoa burudani na kuelimisha watu juu ya kupambana na virusi vya Ukimwi kwa kuonesha filamu, kama vile spider – man, mechi za mpira wa miguu laivu na kutoa huduma ya kupima bila malipo, hivyo tumewalenga zaidi vijana. Ninatoa wito vijana wajitokeze kwa wingi kuja kupima,” alisema Dk. Nyirenda kutoka AMREF.
Dk. Nyirenda alisema maonesho hayo yatafanyika kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Novemba 5, mwaka huu na Novemba 6, mwaka huu uwanja wa Biafra, na mikoa mingine ambayo ni Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Aliongeza kuwa vifaa hivyo vitatumika nchi nzima na huduma hivyo itakuwa ni endelevu.
Kwa upande wa Meneja Mwandamizi wa Sony Corporation, Asako Tomura alisema wametoa Screen kubwa ya inchi 150 na projekta ya ubora wa hali ya juu vyenye thamani ya dola za Marekani 120,000.
Naye Mratibu wa Mfuko wa Dunia kutoka Makao Makuu, Geneva Mai Hosoi alisema hapa nchini kuna idadi ya watu milioni moja wanaoishi na virusi vya Ukimwi, kati yao 450,000 wanahitaji dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV’s) na 250,000 ndio wanaopata dawa hizo kupitia mfuko huo na wafadhili wengine.
Aliongeza kuwa licha ya upatikanaji wa huduma hivyo kuimarika nchini kwa kiasi kikubwa lakini bado kuna watu wengi wanaoihitaji.
Dk. Hiltruda Temba, ambaye ni Mratibu wa mfuko huo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliishukuru Sony kwa kutoa vifaa hivyo ambayo vitaongeza kasi ya mapambano ya ugonjwa huo.
“Tunaomba watu wajitokeze kupima ili kuweza kuingia mapema katika huduma za tiba wakati kinga iko juu, kwani takwimu zinaonesha kuwa watu wanachelewa kuingia katika huduma za tiba,” alisema Dk. Temba.