Dk. Mgimwa Aishauri IMF Kupunguza Masharti ya Mikopo

Waziri wa Fedha Mhe William Mgimwa akitoa maelekezo kwa Msemaji wa Wizara ya Fedha Bi. Ingiahedi Mduma, Kamishina Msaidizi wa Fedha za Nje, Jerome Bureta na Ofisa mwandamizi, Omary Khama Jijini Tokyo-Japan. (Picha na Scola Malinga)

Waziri wa Fedha, William Mgimwa akiongoza Mkutano wa wananchama wa kundi la kwanza la Afrika katika mkutano wa IMF Jijini Tokyo-Japan

Na Mwandishi Maalumu, Tokyo Japan

WAZIRI wa Fedha nchini Tanzania, William Mgimwa amelishauri Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kupunguza masharti magumu ikiwa ni pamoja na shirika hilo kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo nafuu ili nchi zinazoendelea ziweze kunufaika zaidi.
Waziri Mgimwa alitoa ushauri huo alipokuwa akishiriki katika kikao cha kundi la Africa (African Group one Constituency) kinachofanyika jijini Tokyo nchini Japan.
“Shirika la fedha la kimataifa (IMF) hujishughulisha na kutoa ushauri wa kisera kwa nchi wanachama na kutoa mikopo na misaada ya kifedha…jambo kubwa ni kuangalia jinsi ya kuboresha taratibu za kukopesha katika mikopo nafuu,” alisema Waziri Mgimwa.

Waziri Mgimwa akitoka kwenye mkutano na ujumbe alioambatana nao katika Mikutano ya IMF Jijini Tokyo- Japan. Picha na Scola Malinga

Waziri Mgimwa aliwasilisha hoja kwa niaba ya Magavana wa Afrika, na mbele ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Shinowara, na kulitaka shirika hilo kupunguza kiwango cha kigezo cha kukopa ili kuruhusu nchi zinazoendelea kupata unafuu na kuziwezesha kukopa fedha za kufadhili kwa miundombinu ya Barabara, Reli na Bandari.
Mgimwa alisema kuwa, mkutano huo uliangalia uhalisia na vigezo vinavyotolewa na Shirika la Fedha la kimataifa kuruhusu nchi wanachama kukopa tu katika ukomo wa sasa wa asilimia 35 na zaidi (Concesionality).
Aliendelea kufafanua kwamba, jambo kubwa ni kuangalia jinsi ya kuboresha taratibu za kukopesha katika mikopo nafuu. Aidha, wajumbe wa mkutano wamekubaliana na haja ya kuwepo kwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa nchi zote zinakuwa na madeni yanayohimilika”. Alisisitiza Mgimwa.
Aidha wakijadiliana katika mkutano huo wajumbe hao wameshauri Shirika la fedha la kimataifa pamoja na taratibu zake, liangalie namna ya kulegeza masharti ya mikopo ili nchi wanachama ziweze kuboresha miundombinu.
“IMF walau itizame aina ya miradi yenye chachu ya ukuwaji wa uchumi ambayo inaweza kutizamwa kwenye viwango vya ukopaji vya chini ya asilimia 35”. Aliongeza Mgimwa.
“Tunashukuru kuwa IMF imekuwa ikitupatia mikopo ya masharti nafuu, mikopo ile ya mapumziko ya miaka saba kabla ya kuanza kulipa na yenye riba ndogo sana na yenye masharti nafuu”. Mgimwa alisisitiza.
Alitolea mfano wa mradi wa gesi wa Tanzania, Mgimwa alisisitiza kuwa upatikanaji wa gesi utaongeza uzalishaji, ajira na viwanda. Kuongezeka kwa ajira kutaongeza kukua kwa pato la Taifa. Hii itasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa nchi ya Tanzania na hata Afrika kwa ujumla. Mikutano hiyo bado inaendelea hapa jijini Tokyo-Japan na nchi wanachama wanaendelea kuja kwa wingi.