WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema anaamini kwamba uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani unaoendelea nchini kote leo, utafanyika wa amani na utulivu. Akizungumza mara baada ya kupiga kura leo asubuhi Oktoba 25, 2015 katika kijiji cha Kibaoni, wilaya ya Mlele, mkoa wa Katavi, Waziri Mkuu Pinda amesema hali aliyoiona tangu asubuhi inatia
matumaini.
Waziri Mkuu ambaye alipiga kura leo saa 3:10 asubuhi, alisema: “Watu wamejitokeza kwa wingi. Ninawasihi Watanzania waendelee kumuomba Mungu ili uchaguzi umalizike kwa amani. Lakini zaidi tuendelee kumuomba
Mungu ili amani tuliyonayo iendelee kudumu,” alisema.
Akizungumzia hali aliyoikuta kwenye kituo chake cha kupigia kura, Waziri Mkuu alisema amefurahi kuona utaratibu mzuri uliopangwa wa kutenganisha wapigakura. “Nimekuta akinamama wana mistari yao,
akinababa wana mistari na hapa kituoni kuna sehemu nne za kupigia kura,” alisema.
Alisema kwa wastani mtu mmoja anatumia dakika mbili tangu kuhakikiwa hadi kupiga kura. “Hii ni dalili njema kuwa kuna utaratibu mzuri na kwamba watu watamaliza mapema kupiga kura,” alisema.
Aliwataka wapigakura kote nchini wakimaliza kupiga kura waende majumbani kwao ikiwa ni kuitikia maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanayowataka wananchi wasifanye mikusanyiko mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura.
Naye msimamizi wa kituo hicho ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Kibaoni, Bw. Thomas Senga alisema watu wamejitokeza mapema tangu saa 1 asubuhi. Alipoulizwa endapo mtu aliyesahau shahada yake lakini jina
lake lipo kwenye orodha ya waliojiandikisha ataruhusiwa kupiga kura, alijibu kwamba mtu wa aina hiyo hataruhusiwa kupiga kura.