Dk. Magufuli awakoromea Makandarasi

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akiwa ziarani Igunga na makandarasi.

*Aanza utekelezaji ahadi ya ujenzi wa daraja Igunga

Na Martin Ntemo, Habari- Wizara ya Ujenzi

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli (Mb), ametoa onyo kali kwa wakandarasi ambao wamesitisha kazi za ujenzi wa miradi ya barabara hasa ile ya maendeleo kwa kisingizio cha kutokamilishiwa kwa malipo ya awali.

Magufuli aliyasema hayo hivi karibuni akiwa ziarani katika wilaya za Nzega na Igunga wakati alipokutana na viongozi anuai wa Mkoa wa Tabora pamoja na wakandarasi ambao wako mkoani humo wakijenga barabara.

Jumla ya miradi mitano ya barabara na mradi mwingine kutokea mkoani Singida iko katika hatua mbalimbali za ujenzi kwa kiwango cha lami mkoani hapo. Miradi hiyo ni pamoja na Nzega – Puge km 59, Puge – Tabora km 56, Tabora – Nyahua km 85, Tabora – Ndono km 42, Ndono – Urambo km 52 na Manyoni – Itigi – Chaya km 89.

Awali akimkaribisha Waziri huyo katika mkutano uliowakutanisha watendaji kutoka Tanroads; Uongozi wa Mkoa wa Tabora na Wakandarasi wanaojenga barabara mkoani humo, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Moshi Chang’a alimshukuru Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wilayani humo wakati akimnadi mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Peter Kafumu kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema anasikitishwa na kasi ndogo ya utendaji wa baadhi ya wakandarasi mkoani Tabora. “Changamoto tuliyonayo ni kasi ndogo ya utekelezaji na unapofuatilia makandarasi hawa wanadai kuwa hawana fedha kutokana na madai yao kutolipwa,” alisema Chang’a.

Aidha Mtendaji Mkuu wa Tanroads Eng. Patrick Mfugale kwa upande wake alitofautiana na visingizio vilivyotolewa na Wakandarasi vya kutolipwa mapema fedha zao na kudai kuwa wengi wamesha lipwa na kiasi wanachodai ni kidogo.

Alisema wakandarasi wote walikuwa wanadai wastani wa sh. bilioni 10 kila mmoja na tayari wote wamelipwa sehemu kubwa ya fedha hizo huku wakiwa wamebakiza kiasi cha sh. bilioni moja moja tu kwa kila mkandarasi. “Kiasi hicho ni kidogo sana kukitumia kama kigezo cha kuchelewesha kazi,” alisema Eng. Mfugale.

“Hata kisingizio cha uhaba wa maji pia hakiwezi kuwa sababu kwani kabla ya mkandarasi yeyote hajaomba kazi hutakiwa kuyafahamu vizuri mazingira ya eneo hilo ili ajihakikishie kuwa anajumuisha gharama zote za utekelezaji katika zabuni yake, sasa hili la maji linatokea wapi katika hatua hii” alihoji Mfugale.

Kwa upande wake Mheshimiwa Magufuli, hakukubaliana na malalamiko ya wakandarasi na akawaonya wahandisi wasimamizi kutoshirikiana na Wakandarasi wanao wasimamia katika kutengeneza mazingira ya kuongeza gharama za miradi ambayo hugharimu fedha nyingi zinazotokana na kodi za wananchi.

Aliafikiana na Mtendaji Mkuu wa Tanroads kuwa fedha za awali zimelipwa na hivyo kuwaasa Wakandarasi wote kuhakikisha wanaendeleo na kazi bila ya visingizio vyovyote. “Haiwezekani kuambiwa kuwa hakuna maji wakati katika taarifa ya Mkuu wa Mkoa tumeelezwa yapo madaraja 284 katika mkoa huu, hivi haya madaraja huwa yanapitisha nini,” alihoji Magufuli.

Waziri Magufuli aliwataka wakandarasi hao kurejea kazini mara moja na kumalizia majukumu yao ndani au hata kabla ya muda wa mkataba kwani, kinyume na hapo hatua kali dhidi yao zitachukuliwa kwa mujibu wa mikataba yao.

“Kusimama kufanya kazi inaonyesha kuwa wakandarasi hao hawana uwezo na hili litanishangaza kwani utawezaje kuomba kazi za mabilioni halafu usimamishe kazi kwa madai hayo madogo,” alisisitiza Magufuli.

Wakati huo huo Waziri Magufuli kwa niaba ya Serikali aliwahakikishia Wakandarasi hao pamoja na Uongozi wa Mkoa madai yao yamepokelewa na yatalipwa na zoezi hilo linaanza hivi karibuni.

“Nasema fedha zenu zitalipwa na wale wote mliosimamisha mradi nawataka mrudi kazini mara moja na hakuna sababu ya kudai kumaliziwa fedha wakati kazi zenyewe bado hamjakamilisha kwa fedha mlizokwishapewa,” alisema Magufuli.

Dk. Magufuli alisema kuwa Serikali imeingia mikataba ya kiasi cha Sh. bilioni 425 kwa ajili ya miradi sita ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami itakayounganisha makao makuu ya mkoa huo wa Tabora na mkoa wa Singida, Kigoma na Shinyanga kupitia Nzega.

Hata hivyo, Waziri Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads kuhakikisha wanaacha kuwarundikia kazi wakandarasi wachache na akatolea mfano wa baadhi yao wana miradi zaidi ya 10 mikubwa lakini bado wanatishia kusimamisha kazi, jambo ambalo haliwezi kuendelea kuangaliwa bila ya kuchukuliwa hatua. “Wakandarasi wenye kazi nyingi kwa sasa wasipewe kazi nyingine hadi watakapo kamilisha walizo nazo,” aliagiza Magufuli.

Akizungumzia usimamizi wa fedha za barabara Dk. Magufuli alisema baadhi ya halmashauri za Wilaya zimebainika kuwa na matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

Alitolea mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kwamba katika mwaka wa fedha ulimalizika ilishindwa kutumia zaidi ya Sh. milioni 100 za matengenezo ya barabara licha ya kwamba baadhi barabara zake zinaelezewa kutopitika wakati hata fedha hizo hazijulikani zimehifadhiwa katika akaunti ya nani.

“Wakurugenzi ambao wanatumia fedha vibaya au hawataki zitumike kinachotakiwa ni kuandika barua na kuziwakilisha kwa waliowateua ili wapongezwe kwa matumizi mabaya ya fedha hizo za barabara” alisema Dk. Magufuli.

Baada ya kikao hicho na watendaji, Dk. Magufuli alipata fursa ya kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyikia katika Uwanja vya Sokoine hapo hapo wilayani Igunga, ambapo aliwatambulisha wakandarasi ambao wanakwenda kutembelea eneo la daraja la Mbutu kwa madhumuni ya kukamilisha zabuni za ujenzi huo.