Dk. Magufuli atunukiwa uanachama wa heshima wa Taasisi ya Wahandisi

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (kushoto) akipokea cheti kutoka kwa Rais wa IET Eng Dk. Malima Bundala

TAASISI ya Wahandisi Tanzania (Institution of Engineers Tanzania – IET) imemkabidhi Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli (Mb) Cheti cha Uanachama wa Heshima ya Juu ya Taasisi hiyo.

Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Injinia Dk. Malima Bundala alimkabidhi Magufuli cheti hicho baada ya kutangazwa rasmi kwamba ametunukiwa heshima hiyo kubwa katika Mkutano Mkuu wa Wahandisi uliofanyika mapema Desemba mwaka 2011 mkoani Arusha. Uteuzi wa Mwanachama wa Heshima ya Juu hufanywa na Baraza la IET kwa kumtambua mtu yeyote ambaye amethibitika kuchangia kipekee katika uendelezaji wa Taaluma ya Uhandisi kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii.

Waziri Magufuli akipokea cheti hicho alielezea kuwa yeye binafsi hakuona kama anastahili tuzo hiyo lakini kwa vile Taasisi ya Wahandisi imeendelea kumtafuta kwa ajili ya kumkabidhi cheti hicho, hana budi kilishukuru Baraza zima la Taasisi ya Wahandisi kwa heshima hiyo kubwa waliyompa ya kutambua mchango wake katika fani ya Uhandisi.

Magufuli alielezea kuwa Serikali kwa upande wake inatambua umuhimu wa Wahandisi katika ujenzi wa Taifa na ndiyo maana hata Mlezi wa Taasisi hii ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Magufuli alitumia fursa hiyo pia kuipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kuifanya ya kusajili Wahandisi lakini pia kuwachukulia hatua Wahandisi wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo.

Katika hatua nyingine IET imewasilisha pendekezo la kuwepo kwa nafasi ya Mhandisi Mkuu wa Serikali kama ilivyo katika maeneo mengine kama vile uwepo wa Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu, Mganga Mkuu, Mkemia Mkuu na wengineo. Injinia Bundala alieleza kuwa, Mhandisi Mkuu atasaidia kuratibu shughuli mbali za kihandisi zinazotekelezwa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali ipasavyo.

Aidha kuhusu usimamizi wa usalama barabarani Rais wa IET Injinia Bundala alibainisha kuwa ingawa zipo taasisi kadhaa zinahusika na jukumu hilo bado hakuna chombo maalum cha uratibu wake. Taasisi ambazo zimetajwa kuhusika moja kwa moja na suala zima la usalama barabarani ni pamoja na SUMATRA, Kikosi cha Usalama Barabarani katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ujenzi.

Dk. Bundala aliendelea kufafanua kwamba Taasisi ya Wahandisi inatambua jitihada zinazofanywa na Wizara ya Ujenzi za kuanzisha Wakala maalum utakao simamia usalama barabarani hapa nchini. Hata hivyo wanaiomba wizara hiyo kutoa kipaumbele kwa suala hili ili lisichukue muda mrefu kwani athari zinaendelea kutokea barabara zikiwemo ajali na misongamano ya magari mijini ni kubwa kwa jamii na kiuchumi. IET ni Taasisi inayojitegemea iliyoundwa mwaka 1977, ikiwa na lengo la kuimarisha fani ya Uhandisi hapa nchini. Taasisi hii tayari ina jumla ya wanachama 3,000 kutoka katika sekta mbalimbali hapa nchini.