Dk. Magufuli atoa heshima za mwisho kwa muasisi wa CCM Chato

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akiuaga mwili wa Marehemu Misungwi eneo la Tegeta Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato leo ameshiriki kuuaga mwili wa marehemu Constantine Jaha Misungwi ambaye ni muasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Chato.

Shughuli za kuuaga mwili wa marehemu Misungwi zimefanyika jijini Dar es Salaam eneo la Tegeta kabla ya mwili huo kusafirishwa kuelekea Mji wa Chato kwa mazishi.

Akimuelezea marehemu Misungwi mmoja ya watoto wa marehemu, Kaloli alisema kuwa baba yake alilazimika kuletwa Dar es Salaam akitoke Chato kwa ajili ya matibabu ya kansa na mauti yalimkuta nyumbani kwake, ikiwa ni siku mbili mara baada ya kutibiwa Katika Hospitali ya Tumaini ya jijini Dar es Salaam.

Marehemu Misungwi alizaliwa Julai Mosi, 1925 na katika muda wa uhai wake amewahi kushika nyazifa mbalimbali za kisiasa. Marehemu Misungwi ndiye mwanzilishi wa mji wa Chato na katika nyakati tofauti aliwahi kushika nafasi mbali mbali ikiwamo ya Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi katika mji wa Chato, Udiwani na pia Uenyekiti wa Chamba Cha Mapinduzi katika Jimbo la Biharamulo Mashariki.

Marehemu mzee Misungwu ndiye aliyemshawishi Magufuli kujiunga na siasa mnamo mwaka 1990 na baadaye kumchukulia tena fomu za kugombea Ubunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki mwaka 1995 na kushinda kwa mara ya kwanza.