Dk Magufuli Alia Kifo cha Deo Filikunjombe, Kepteni Silaa

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa, mkoani Njombe, Deo Filikunjombe (kulia) enzi za uhai wake akizungumza na wananchi.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa, mkoani Njombe, Deo Filikunjombe (kulia) enzi za uhai wake akizungumza na wananchi.


MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za vifo vya Mbunge wa Jimbo la Ludewa, mkoani Njombe Ndugu Deo Filikunjombe Haule, Kepteni William Silaa pamoja na abiria wengine wawili ambao wameaga dunia Alhamisi, Oktoba 15, 2015 kwa ajali ya helkopta iliyotokea katika eneo la Hifadhi ya Selous mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano CCM Ofisi Ndogo, Lumumba kwa vyombo vya habari, Dk. Magufuli katika salamu za rambirambi alizowatumia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe, Deo Sanga, na Meya wa Manispaa ya Ilala Mstahiki Jerry Silaa, Dk. Magufuli amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya Ndugu Filikunjombe na Ndugu Silaa ambavyo nimetaarifiwa kuwa vimetokea kwa ajali ya helkopta aliyokuwa akiitumia Ndugu Filikunjombe kwa Kampeni zake za Ubunge katika jimbo hilo la Ludewa.
Katika salamu zake hizo za rambirambi Dk. Magufuli ameongeza kuwa: “Kama unavyojua, namfahamu vizuri Ndugu Filikunjombe. Alikuwa Mbunge mwenzangu katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mitano ndani ya bunge letu. Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Ludewa, ambao aliwawakilisha kwa miaka mitano iliyopita akiwa Mbunge wao. Hata nilipofanya ziara ya kampeni katika jimbo lake la Ludewa mwezi uliopita nililala nyumbani kwake, hiyo inaonesha nilivyokuwa karibu naye. Tutakosa utumishi wake mahiri sana.”

Salamu zake za rambirambi kwa Mstahiki Meya Jerry Silaa, Dk. Magufuli amesema: “Nimesikitishwa sana na taarifa ya kifo cha Baba yako Kepteni William Silaa, kwani ni tukio lisilozoeleka. Ni jana tu nimeshiriki nawe katika kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 katika jimbo unalogombea Ubunge, jimbo la Ukonga, naungana nawe katika kipindi hiki kigumu cha msiba mkubwa. Nakupa pole wewe binafsi, familia yenu, ndugu, jamaa na marafiki wote”.

Aidha aliongeza “Nakutumia wewe Ndugu Sanga, Mwenyekiti wetu wa CCM mkoa wa Njombe salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Ndugu Filikunjombe na abiria hao wengine. Aidha, kupitia kwako namtumia rambirambi nyingi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao.”

Dk. Magufuli ameongeza “Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa Jimbo na Wilaya ya Ludewa ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa kipindi chote. Aliwawakilisha vizuri na kujali sana maslahi yao. “

Ametuma pia salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Ndugu Filikunjombe kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi. Amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. Pia naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema peponi roho ya Deo Filikunjombe Haule”. Amen.