Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli amesema hayo leo, Ikulu alipokutana na Ndugu Zhang Ping, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunist cha China (CPC), ambacho ndicho chama tawala nchini humo.
“Tuimarishe uhusiano wetu kwa misingi ya kuufanya uwe uhusiano wa kuisaidia Tanzania kunufaika kiuchumi na kibiashara ili kuweza kutimiza azma yangu ya kuwaletea watanzania maendeleo”. Amesema Rais Magufuli ambaye amekutana na Ndg. Ping aliyekuja nchini kumuwakilisha Rais wa China katika sherehe za kuapishwa Rais Magufuli tarehe 5 Oktoba, 2015.
Rais Magufuli amekutana na viongozi wengine ambao pia waliwakilisha viongozi wa nchi zao katika sherehe hizo.
Wawakilishi hao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Algeria Ndg. Ramtane Lamamra, Ndg. Pascal Nyabenda, Spika wa Bunge la Burundi na Waziri wa Kilimo wa Misri Ndg. Essam Fayed.
Mapema asubuhi Rais Magufuli amemuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ndg. George Mcheche Masaju na kisha kuendelea na kazi zake za kiofisi.
Rais Magufuli amewataka watumishi wote kufanya kazi zao kwa uadilifu, kwa bidii na kujituma zaidi ili kuweza kuwatumikia watanzania na kuweza kutimiza mategemeo yao ya kuletewa maendeleo na kukua kiuchumi.
Wakati huo huo; Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Wizara ya Fedha Novemba 6, 2015.
Katika ziara hiyo Rais alipatafursa ya kutembelea baadhi ya Ofisi za Wizara na baadae kuzungumza na Viongozi wa Wizara ili kufahamu changamoto ambazo zinaikabili Wizara ya Fedha.
Wakati akimkaribisha Rais Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacius Likwelile alimueleza kuwa Wizara ya Fedha inakabiliwa na changamoto kubwa inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani. Miongoni mwa sababu ni misamaha ya kodi, wafanyabiashara wengi hasa wakubwa kukwepa kodi, makusanyo yasiyoridhisha ya maduhuli na kutokulipwa kwa kodi za majengo. Aidha Dk. Likwelile alishauri ni bora kuwekwa mifumo mizuri, ikiwemo matumizi ya Tehama na EFDs.
“Pamoja na ziara yangu kuwa ni ya kustukiza nimefurahi sana kukuta Viongozi wote wapo ofisini na wanafanyakazi. Jambo hili limenipa faraja kubwa. Ziara yangu ya kuja hapa nimejifunza na kujua changamoto zipi zinazowakabili”. Alisema Rais.
Nimesikia changomoto nyingi na ninaagiza kuwa muhakikishe walipakodi wakubwa wanalipakodi na kusimamia kikamilifu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili iwezeze kukusanya kodi kikamilifu na si kuwabana wafanyabiashara wadogo wa dogo.