KITENDO cha Serikali kupanga bei ya pamba ya shilingi 660 kimedaiwa ni manyanyaso kwa wakulima hapa Nchini nakuwafanya kuendelea kuishi maisha duni huku wafanyabiashara wachache wakifaidika kutokana na nguvu za wakulima wanazotumia katika kilimo cha zao hilo.
Kauli hiyo ilitolewa Mjini Musoma na Mbunge wa jimbo la Serengeti (CCM) DK. Stiven Kebwe alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa Gazeti hili Mjini Musoma kutokana na malalamiko yaliyotolewa na wakulima wa zao hilo baada ya kudaiwa kupata hasara kutokana na gharama wanazotumia katika kilimo na bei iliyopangwa kuuzwa.
Dk.Kebwe alisema Serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa ukaribu zaidi kama inawathamini wakulima wa zao la pamba kutokana na bei ya chini iliyopangwa ambayo haina tija kwa wakulima bali kuwafanya kuishi maisha ya hali ya chini licha ya kujituma katika kilimo hicho.
Alisema Serikali ndio iliyowahimiza wakulima kulima zao hilo kwa juhudi kubwa na kuwahaidi kupangwa kwa bei itakayoanzia shilingi elfu moja na zaidi hali iliyowafanya wakulima kujituma mashambani lakini katika hatua ya mavuno imewatupa wakulima na kuwaacha wakiendelea kugandamizwa na wanunuzi wa pamba.
“Kwa hili Serikali ina kila sababu ya kulisimamia kuhakikisha wakulima wanapewa bei ambayo haiwaumizi kwa kuwa wao ndio waliowahimiza wakulima kulima kwa juhudi zao la pamba na ahadi ya bei nzuri sasa ni wajibu kuhakikisha kile kilichoahidiwa kinatekelezwa kwa wakulima.
“Haiwezikani wakulima wetu hususani kule Serengeti ambako kwa kipindi hiki wamejitahidi kulima pamba kutokana na ahadi ya bei nzuri huku wakitumia gharama kubwa katika kununua madawa,pembejeo pamoja na mahitaji ya kuhitunza pamba hiyo kisha waiuze kwa bei ya shilingi 660,”alisema Dk.Kebwe.
Alisema kitendo cha kupanga bei hiyo ni kama manyanyaso kwa wakulima na kina wavunja moyo hasa kutokana na hamasa waliyokuwa wamepewa na Serikali juu ya bei nzuri ambayo wangeuza pamba yao mara baada ya mavuno.
Mbunge huyo wa Jimbo la Serengeti aliongeza kuwa licha ya bei ya chini ambayo haikidhi kutokana na gharama ya kulima zao hilo bado kuna udanganyifu mkubwa katika mizani ambayo inatumiwa na wanunuzi wa pamba kwa wakulima na kupelekea kuendelea kuwakandamiza zaidi.
Alisema Serikali inabidi iimalishe viwanda vya ndani viwe vya kutosha ili pamba inayolimwa hapa Nchini iwezwe kuuzwa hapa hapa na kutumika kutengenezea mali ghafi mbalimbali zitokanazo na zao la pamba.
Aliongeza kuwa zipo mali ghafi nyingi ambazo zinaweza kupatikana kutokana na zao la pamba na kutengenezwa hapa nchini iwapo Serikali itahakikisha inafufua na kuongeza viwanda ambavyo vitakuwa vikinunua pamba ya wakulima kuliko kuishia asilimia kubwa ya kupelekwa nje ya Nchi.