Na Tiganya Vincent, MAELEZ0-Dodoma
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Jumanne Kawambwa amesema katika kipindhi cha miaka mitano ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne umeongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma ngazi mbalimbali kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Dk. Kawamba amesema hayo leo Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Elimu kwenye maonesho ya wakulima ya Nane Nane ambayo kitaifa yanafanyika mjini Dodoma.
Alisema wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani mwaka 2005 kulikuwa na vyuo vikuu 18 vikiwa na wanafunzi 42,000, lakini hivi sasa kuna vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 38, vikiwa na wanafunzi 176,000.
Dk. Kawambwa aliongeza kuwa mwaka 2005 Shule za sekondari zilikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 524,000 lakini hivi sasa kuna zaidi ya wanafunzi milioni 1.6 wanaosoma. Kwa upande wa Shule za Msingi hivi sasa kuna wanafunzi milioni 8 ambao wanasoma katika shule za msingi mbalimbali hapa nchini.
Waziri huyo alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto ambazo Serikali ya Awamu nne imepanga kukabiliana nayo ni kuanza kuzijengea uwezo shule za sekondari za wananchi kwa kuwajengea mahabara na kuwapatia vifaa, kuwajengea makitaba na kuziwekea vitabu vya kutosha.
Aliongeza eneo jingine ambalo limeanza kufanyiwa kazi na serikali ya Awamu ya Nne ni pamoja ya kuongeza idadi ya walimu kwa ajili ya shule hizo pamoja na kuwajengea nyumba walimu ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa walimu.
Alisema lengo hilo ni kutaka kuwavutia walimu wengi kupenda kufundisha maeneo yote na hivyo kuwasaidia vijina kuwa na walimu wa kutosha.
Waziri huyo alisema sanjari na mambo hayo sehemu ya pili ya uboreshaji wa shule za wananchi wapo katika mkakati wa kuboresha masilahi ya walimu ili wavutiwe kufanyakazi katika mazingira yote.