Dk. Kawambwa awaonya wamiliki vyuo vya uwalimu

Na Tiganya Vincent, MAELEZO-Dodoma

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Jumanne Kawambwa amewaonya wamiliki wa vyuo vya ualimu binafsi kuacha kuwadanganya vijana waliomaliza kidato cha nne kuwa wanaweza kujiunga na masomo ya Stastahada (Diploma) kwa sifa za kidato cha nne kwa kuwa na pasi tano.

Dk. Kawambwa alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda la Wizara ya Elimu kwenye maonesho ya wakulima ya Nane Nane mjini Dodoma.

Alisema kuwa katika mfumo wa kuandaa walimu ya Cheti unamtaka awe ameliza kidato cha nne na amepata alama zilizopungua 28 na Diploma atakakiwa awe amemaliza Kidato cha Sita, hivyo kusema kuwa mwanafunzi aliyemaliza Kidato cha Nne bila kujiendeleza anaweza kuchukua Diploma ni kuwadaganya wananchi.

Alisema kuwa hatua hiyo imekuwa ikisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wazazi na watoto pindi wanapokataliwa kufanya mitihani ya kumaliza masomo yao kwa kukosa sifa na Baraza la mitihani.

Dk. Jumanne alionngeza kuwa hakuna utaratibu wa kujiunga na Diploma ya ualimu moja kwa moja kwa mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne pasipo kufuata taratibu zinazotakiwa ili apate sifa ya kujiunga na Vyuo vya Ualimu kwa ngazi za Diploma.

Alisema kuwa Wizara ya Elimu itachukulia hatua wamiliki na Vyuo vya Ualimu vinavyodanganya wananchi kwa ajili kujipatia fedha hali wakijiua kuwa mwanafunzi huyo hataruhusiwa kufanya mitihani ya mwisho watafutiwa usajili na adhabu nyingine. Dk. Kawambwa alisema kuwa wameshawahi kuchukulia hatua vyuo mbalimbali ambavyo vilikiuka taratibu za usajili wanachuo.

Aidha Waziri huyo aliwaagiza wakaguzi wa Elimu katika mikoa yote kuhakikisha wanakagua vyuo vya ualimu nchini ili kuhakikisha kuwa wamesajili wanachuo wenye sifa ili kuepuka kuzalisha walimu ambao hawawezi kuwasaidia vijana.

Awali akitoa maelezo kwa Waziri wa Elimu alipotembelea maonyesho ya wakulima ya nanenane ya mjini Dodoma Ofisa Elimu Mkuu kutoka Wizara ya Elimu Jane Kamwera alimweleza kiongozi huyo kuwa katika maonyesho hayo wapo vijana walimweleza kuwa kuna vyuo vya watu binafsi vimekuwa vikiwaambia kuwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne wanaweza kujiunga na Diploma ya Ualimu ili mradi awe amefaulu masomo matano.

Alisema kuwa hali hiyo imesababisha malalamiko mengi kwa sababu wamekuwa wakipoteza muda Vyuoni na mwishoni wanakataliwa kufanya mitihani ya Taifa.