Balozi wa Japan nchini, Mh. Masaki Okada (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hussein Kidanto wakitiliana saini mkataba wa fedha za ruzuku shilingi milioni 70/ zilizotolewa na serikali ya Japan kwa ajili ya kununua magari mawili ya wagonjwa (Ambulance). Tukio hilo lilishuhudiwa na viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo aliyemaliza muda wake Dkt. Marina Njelekela.
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli ameishukuru Japan kupitia Balozi wake alioko nchini kwa kusaidia miradi inayochangia maendeleo ya moja kwa moja hususani afya, elimu na maji. Dk. Magufuli alisema hayo jana katika makazi ya Balozi wa Japan Nchini, Masaki Okada yaliyopo Masaki Jijini Dar es Salaam wakati wa kutiliana na saini za mkataba wa fedha za ruzuku zitakazoenda kusaidia maendeleo kwa jamii ikiwemo Jimbo la Chato na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika hafla hiyo, Dk. Magufuli aliambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya ya Chato, pamoja na Wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwemo Mkurugenzi wa zamani wa hospitali hiyo Dk. Marina Njelekela pamoja na wa sasa Dk. Hussein Kidanto.
Balozi Okada na Mkurugenzi Dkt. Kidanto wakibadilishana hati za mikataba hiyo.
Dk. Magufuli alishuhudia utiaji wa saini wa mikataba hiyo ambapo Balozi Okada alitoa kiasi cha sh milioni 70, kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kisasa ya kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo mpaka sasa inadaiwa wana Ambulance moja pekee.
Mbali na kiasi hicho cha fedha, Pia Dk. Magufuli alishuhudia utiaji wa saini huo ambapo Balozi huyo alitoa sh milioni 165, kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kukamulia mafuta ya Alizeti yenye viwango vya Kimataifa.
Dk. Magufuli alishukuru kwa niaba ya Serikali na pia akiwa kama Mbunge wa Chato, alisema Japan imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia juhudi za maendeleo kwa wananchi mbalimbali wa mijini na vijijini.
Hata hiyvo Dk. Magufuli alishtushwa na hali ya Hospitali hiyo ya Taifa kuwa na Ambulance moja pekee wakati wao Halmashahuri ya Chato hadi sasa wameweza kuwa na Ambulance tatu.
Balozi wa Japan nchini, Mh. Masaki Okada (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, Ndugu Clement Berege wakitiliana saini mkataba wa fedha za ruzuku shilingi milioni 165 kwa ajili ya kujengea kiwanda cha kukamulia mafuta ya Alizeti wilayani Chato mkoani Geita.
“Nimeshtushwa sana na hili la kusikia kuwa mna Ambulance moja pekee. Yaani hata Chato pale tuna Ambulance tatu. Naomba Mkurugenzi mpya, uendelee kuomba kwa mabalozi wengine ili tuweze kupata Ambulance nyingi zaidi pia wanahabari mtusaidie kwa hili.” Alisema Dk. Magufuli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chato, alipogeza Japan, kwa msaada wao kwani utaenda kusaidia Halmashauri ya Chato kama ulivyokusudiwa.
“Wakazi wa Chato ni wakulima, wafugaji na wavuvi, hivyo kwa msaada huu pia utakuwa chachu ya maendeleo hasa kwa kilimo cha Alizeti.” Alisema Mkurugenzi huyo.
Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akitoa shukrani kwa serikali ya Japan inayowakilishwa na Balozi Masaki Okada baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya fedha za ruzuku shilingi milioni 235 sawa na dola za Kimarekani 136,015 zilizotolewa na serikali ya Japan.
Japan imekuwa ikisaidia mara kwa mara wilaya ya Chato, ambapo mwaka 2013, Japan walitembelea huko na kujionea shida mbalimbali kwa wakulima wa Alizeti hivyo wameona kusaidia msaada huo.
Mbali na kusaidia mashine hiyo ya Alizeti Japan pia imekuwa ikisaidia maendeleo mbalimbali ikiwemo shule za msingi, Sekondari na huduma za afya kwa Hospitali iikwemo wodi ya akina mama.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Bw. Rodrick Mpogolo akizungumza kwenye hafla hiyo ambapo pia alimshukuru Balozi Mh. Masaki Okada kwa kutengeneza ajira wilayani kwake kupitia msaada huo.
Pichani juu na chini ni baadhi ya wageni waalikwa na waandishi wa habari waliohudhuria hafla hiyo fupi iliyofanyika nyumbani kwa Balozi Mh. Masaki Okada jana jijini Dar.
Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akiteta jambo na Balozi wa Japan nchini, Mh. Masaki Okada mara baada ya hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba ya fedha za ruzuku kwa ajili ya kuendeleza miradi inayochangia maendeleo ya moja kwa moja nchini.
Waziri wa Japan nchini, Mh. Masaki Okada akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mara baada ya kuhitimisha zoezi la utiaji saini wa mkataba wa fedha za ruzuku kwa ajili ya kununua magari mawili ya wagonjwa (Ambulance) zilizotolewa na serikali ya Japan.
Balozi wa Japan nchini, Mh. Masaki Okada katika picha ya pamoja na Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli pamoja na viongozi wa halmashauri ya Chato.
Chanzo: modewjiblog