SERIKALI imesema licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi zaidi, utajiri mkubwa na mazao na bidhaa mbalimbali ambazo zina soko nchi za nje, lakini bado inakabiliwa na changamoto ya namna ya kuzitumia fursa hizo.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, kwenye Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa ‘Saba Saba’ na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal alipokuwa akifungua rasmi maonesho hayo.
Dk. Bilal alisema hata hivyo zipo fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kibiashara hasa za nje. Alizitaja fursa hizo ni pamoja na zile zilizotolewa chini ya mfumo na utaratibu wa mpango wa AGOA, EBA (Everything But Arms), EPA, mahusiano ya china na Soko la Canada na ile ya kuuza bidhaa katika nchi za China, India na Japan.
Aliwataka wafanyabiashara kuzitumia fursa hizo ili kuweza kujiendeleza wao pamoja na taifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wafanyabiashara wanauza bidhaa zao nje zikiwa zimefungwa ili kuweza kuziongezea thamani.
Alisema uuzaji wa mazao moja kwa moja nje ya nchi badala ya bidhaa halisi umelikosesha taifa kiasi kikubwa cha fedha kwani mara nyingi bei za bidhaa hizo zimekuwa zikishuka katika somko la dunia.
Aidha aliwataka wafanyabiashara mbalimbali wanaoshiriki katika maonesho ya mwaka huu kuweza kujifunza mbinu anuai za kibiashara kutoka kwa wageni jambo ambalo litawaongezea ujuzi na kubadilika kulingana na mabadiliko ya teknolojia.
“…Nchi yetu bado inauza mazao, na bidhaa nyingine kwenda nje, zikiwa bado ni malighafi bila ya kuziongezea thamani. Hali hii ndio imelifanya taifa kuendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa, pale bei za masoko hayo zinaposhuka katika soko la dunia,” alisema Dk. Bilal.
Hata hivyo, alisema Serikali itaendelea kujenga mazingira ya kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani kufanya vizuri zaidi katika biashara zao ili waweze kunufaika na hatimaye taifa kwa ujumla.
Dk. Bilal ambaye katika hafla hiyo pia alifanya uzinduzi rasmi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), aliipongeza mamlaka hiyo kwa kazi inayoifanya, kwani imekuwa ikifanikiwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya washiriki wa ndani na nje kwa kila mwaka.
Hata hivyo Dk. Bilal alitoa zawadi na vikombe kwa washindi mbalimbali wa jumla na makundi waliofanya vizuri katika maonesho hayo baada ya kuteuliwa na kamati maalumu iliyotembelea mabanda.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami alisema maonesho ya Biashara Kimataifa yamekuwa yakifanikiwa kila mwaka kwa kuongezeka washiriki na mapato katika uuzaji wa bidhaa.
Alisema kwa mwaka uliopita mauzo ya ndani kwa taasisi na kampuni yalifikia kiasi cha sh. bilioni 141, huku mauzo ya nje yakipanda maradufu tofauti na miaka iliyopita.