Dk Bilal Katika Maadhimisho Siku ya Mazingira Duniani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya mshindi wa tatu katika usimamizi wa usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya mshindi wa tatu katika usimamizi wa usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR

HOTUBA YA MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI, TAREHE 5 JUNI, 2015 MKOANI TANGA

Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (Mb),
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira;

Mhe. Samia S. Hassan (Mb),
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano;

Mhe. Dkt. Seif Rashid (Mb),
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;

Mhe. Stephen Masele (Mb),
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais;

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

Mhe. Lut. (Mst) Chiku Galawa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

Mhe. Magalula S. Magalula,. Magalula S. M
Mkuu wa Mkoa wa Tanga;

Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga;

Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga;

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo;

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Waheshimiwa Madiwani;

Viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa;

Viongozi wa Dini na Madhehebu mbalimbali mliopo;

Ndugu Wanahabari;

Wageni Waalikwa;

Ndugu Wananchi;

Mabibi na Mabwana.

Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na afya njema, na kuweza kukusanyika hapa siku ya leo, kushuhudia tukio hili muhimu.

Nitumie fursa hii kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Tanga, mikoa ya jirani, na wadau mbalimbali walioshiriki kwa njia moja au nyingine katika kufanikisha Maadhimisho haya. Hongereni Sana!

Aidha, niwashukuru pia kwa mapokezi mazuri na moyo wa ukarimu, mliouonesha kwangu na ujumbe wangu, tangu tulipowasili hapa. Asanteni Sana!

Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Leo Watanzania tunaungana na jamii ya kimataifa Duniani kote kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mazingira. Siku hii muhimu huadhimishwa kwa lengo la kukumbushana na kuelimishana umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira, na wajibu wa jamii kutunza na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kitaifa, Maadhimisho haya yanafanyika hapa mkoani Tanga ambapo Watanzania kote nchini, mikoani, wilayani na vijijini wanaungana kwa pamoja kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuelimishana na kuhamasishana juu ya umuhimu wa kutunza na kuyahifadhi wa mazingira. Ujumbe wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu unasema: “Ndoto Bilioni Saba. Dunia Moja. Tumia Rasilimali kwa Uangalifu.” (Seven Billion Dreams. One Planet. Consume with Care). Kitaifa ujumbe huu unahimiza jamii kutambua umuhimu wa utumiaji endelevu wa rasilimali zetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Idadi ya watu duniani kwa sasa imefikia takriban watu bilioni 7 na inakadiliwa kufikia bilioni 9.6 ifikapo mwaka 2050. Ongezeko la sasa la watu duniani ni changamoto kubwa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya mshindi wa kwanza katika usimamizi wa usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya mshindi wa kwanza katika usimamizi wa usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR


Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina watu milioni 44.9 ambao wanategemea na wataendelea kutegemea rasilimali za mazingira ambazo zinapungua siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali. Hivyo, ujumbe wa mwaka huu unatueleza dhahiri kwamba dunia yetu hii imeelemewa na mahitaji ya binadamu, ni muhimu kwa asasi mbalimbali na wananchi kwa pamoja tukatafakari kwa kina maudhui ya ujumbe huu ili kubuni mbinu za kuendesha shughuli zetu kwa kutumia rasilimali hizo kwa uangalifu na kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Ndugu Wananchi;
Tunafahamu kwamba, uharibifu wa Mazingira ni tatizo kubwa kote duniani linalosababishwa pamoja na mambo mengine na changamoto ya ongezeko la watu na shughuli zisizoendelevu za kijamii na kiuchumi anazofanya binadamu katika jitihada za kujiletea maendeleo.

Matatizo ya mazingira yapo katika maeneo mengi ya uzalishaji katika nchi yetu. Matatizo haya ni pamoja na uharibifu wa ardhí, ukataji wa miti ovyo na uharibifu wa misitu, upotevu wa bioanuai, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa mifumo ya ikolojia, kupungua kwa ubora na upatikanaji wa maji, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili yakiwemo mafuriko ya mara kwa mara yanayosababisha madhara makubwa katika baadhi ya maeneo, maisha ya watu, mifugo na mali zao zimepotea kutokana na athari hizo. Aidha, matatizo mapya yanayojitokeza kwa sasa ni pamoja na kuongezeka kwa taka zitokanazo na vifaa vya umeme na kielektroniki, viumbe vamizi vigeni, viumbe vilivyofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki na mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya kilimo cha biofueli na athari zake. Ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na kutumia rasilimali zetu kwa njia endelevu, ni muhimu tuchukue hatua stahiki za kutunza, kuhifadhi mazingira na kutumia rasilimali zetu kwa njia endelevu.

Serikali imeweka Sera, Mikakati na Sheria za kukabiliana na matatizo haya nchini. Tunaendelea na hatua za kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa mambo haya. Ni muhimu sote tukaongeza nguvu katika utekelezaji wa Mikakati na Sheria zote za mazingira. Mipango ya maendeleo katika ngazi zote izingatie masuala ya hifadhi ya mazingira. Hili ni jambo la lazima kwa nchi yoyote kupata maendeleo endelevu.

Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Pamoja na juhudi zilizochukuliwa kukabiliana na uharibifu wa mazingira ni muhimu ifahamike kwamba mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu, na ndio uhai wa kila kiumbe duniani. Maisha ya binadamu hayawezi kuwepo bila ardhi, maji, mimea na hewa. Pamoja na umuhimu huo, tunaendelea kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo kisichoendelevu kinachofanyika katika vyanzo vya maji, kwenye vilele na miteremko mikali ya milima, matumizi mabaya ya dawa za kilimo, mifugo na viwanda, kilimo cha umwagiliaji kisichoendelevu, matukio ya moto kichaa na uchomaji moto misitu, uchimbaji wa madini usioendelevu na mlundikano wa taka katika maeneo ya mijijni na makazi ya watu. Vile vile, wingi wa mifugo inayozidi uwezo wa malisho husababisha upungufu wa maji na malisho na hivyo kuchangia kuongezeka kwa migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya usimamizi wa usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Kpt . Chiku Galawa wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya usimamizi wa usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Kpt . Chiku Galawa wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Picha na OMR


Ndugu Wananchi;
Sote kwa pamoja tunao wajibu mkubwa wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya mazingira yanayokabili nchi yetu, kila mmoja wetu kwa nafasi yake. Aidha, baadhi ya matatizo haya yanahitaji mikakati ya kudumu katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii za binadamu haziathiri mazingira yetu. Kila mtu awajibike kwa kutunza rasilimali zilizopo; mfano, kutumia nishati mbadala kama biogas, nishati ya jua, upepo na matumizi endelevu ya kuni na mkaa kwa kutumia majiko banifu yanayotumia kiasi kidogo cha kuni na mkaa. Vile vile turejeleze taka za plastiki ili kupunguza kiasi cha taka tunazozalisha ambapo nyingi huingia katika mazingira kwa sababu haziozi.

Aidha, tuendelee na jitihada zifuatazo:-
i) Kuhifadhi ardhi na kupanda miti;
ii) Kudhibiti uchomaji moto ovyo;
iii) Kuhifadhi vyanzo vya maji, milima na misitu ya asili;
iv) Kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya makazi na viwandani;
v) Ujenzi na matumizi ya vyoo bora;
vi) Kudhibiti kilimo na uchimbaji madini usioendelevu;
vii) Kudhibiti matumizi mabaya ya dawa za mifugo na kilimo;
viii) Kusimamia uzalishaji bora usiochafua mazingira kwenye viwanda vyetu;
ix) Kubuni na kutumia tekinolojia na mbinu zinazopunguza uchafuzi wa mazingira katika michakato ya uzalishaji viwandani na katika matumizi ya nishati;
x) Kuendeleza tafiti zinazoweka hifadhi ya hali ya mazingira na mbinu za kukabiliana na uhalibifu wa mazingira nchini; na
xi) Kuyahifadhi mazingira ya maeneo ya pwani, bahari, mito, maziwa na mabwawa, ili kulinda rasilimali hizi na hivyo kuongeza uzalishaji wake.

Ndugu Wananchi;
Kazi ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira unahitaji ushirikiano wa wadau wote kwa ngazi zote. Nitoe wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia tusaidiane katika hili. Watendaji wote katika ngazi zote hatuna budi kushirikiana katika kutekeleza kwa ukamilifu Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira. Mtakapofanya hivyo mtapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira. Aidha, katika kila ngazi pawepo Mipango bora ya ardhi, Mikakati bora ya kudhibiti uvuvi haramu, Mikakati ya kudhibiti uvunaji holela wa misitu na ufugaji usio endelevu. Wizara na Taasisi husika kwa kushirikiana na jamii yote, ziendeleze mafanikio yaliyokwishapatikana kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Mikakati, Mipango, Sheria na Kanuni tulizojiwekea.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata utepe kuzindua rasmi Filamu ya Mamba wa Zigi, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Kushoto kwake ni Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Binilith Mahenge, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata utepe kuzindua rasmi Filamu ya Mamba wa Zigi, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, zilizofanyika kwenye wa Viwanja Vya Tangamani, mkoano Tanga, Juni 5, 2015. Kushoto kwake ni Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Binilith Mahenge, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu. Picha na OMR


Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kujitokeza kushiriki Mashindano ya Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Kupanda na Kutunza Miti kwa Mwaka 2016 ambapo tuzo hiyo itatolewa kwa washindi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni 2016. Aidha, nitumie fursa hii pia kuwakumbusha kuwa mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo ni haki na wajibu wa kila mwananchi kutumia haki yake ya msingi kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Nawahamasisha wananchi wote wenye sifa stahiki kujitokeza kwa wingi katika mchakato mzima wa uchaguzi, ili mtumie haki yenu ya msingi ya kidemokrasia kwa maendeleo ya Taifa letu.

Ndugu Wananchi;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, kwa mara nyingine, napenda kuushukuru na kuupongeza Uongozi wa Mkoa wa Tanga kwa maandalizi mazuri ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira kitaifa. Nazipongeza tena Halmashauri, Taasisi, Kampuni, Vikundi na Watu binafsi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha maadhimisho haya.

Napenda niwakumbushe jambo moja muhimu sana, katika kufanikisha suala zima la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira yetu, ili tufanikiwe ni; “Lazima tuifanye kila siku iwe ni Siku ya Mazingira. Tuchukue Hatua Kukabiliana na Ongezeko la watu, Tutunze Mazingira yetu na Tutumie Rasilimali zetu kwa Uangalifu.“

Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa na taadhima, natamka rasmi kwamba Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yamefikia Kilele.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.