Na Mwandishi Maalum
Instabul
TANZANIA imetoa wito kwa nchi tajiri kutambua nafasi yao katika kuzikwamua nchi masikini ili ziweze kukuza uchumi wake na kuwasaidia wananchi waliomo katika nchi hizo.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal wakati akihutubia mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa unaojadili maendeleo ya nchi masikini nchini Uturuki.
Dk. Bilal alisema mataifa masikini yametekeleza mambo mbalimbali ambayo yameshauriwa na mataifa makubwa sambamba na mashirika ya kimataifa, lakini kikwazo kimebakia katika nafasi za mataifa makubwa kutimiza ahadi zao za kuzikwamua nchi masikini katika umasikini.
“Kama ambavyo ripoti mbalimbali zinavyoonyesha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa kwa muongo wa mwaka 2001 -2010, nchi maskini zimemudu kutimiza
malengo yao mengi, kama sio makubaliano yote yaliyotolewa na nchi tajiri kwa nchi maskini. Jambo linalokatisha tamaa ni hali ya nchi tajiri kutotimiza ahadi wanazotoa,” Dk. Bilal alisema.
Alitolea mfano kwa Tanzania, Dk Bilal alizielezea nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa tangu kupitishwa kwa Azimio la Brussels mwaka 2001, Tanzania ilibadili sera zake nyingi zikiwemo zile zilizolenga kupunguza umasikini.
Aliongeza nchini ilianzisha programu ya MKUKUTA, pamoja na kuweka vyombo vya kusimamia ukuzaji wa uchumi, ikaongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya maamuzi, ikaanisha chombo cha kupambana na rushwa huku pia ikitoa uhuru kwa vyombo vya habari.
Dk. Bilal aliendelea kufafanua kuwa, Tanzania katika kipindi hicho imeongeza uwazi katika mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali, imefanikiwa kupitia upya mikataba ya madini na imefanikiwa kwa kiwango
kikubwa kwa kutumia uwezo wake wa ndani kutanua wigo wa demokrasia nchini.
“Bado ipo haja kwa nchi masikini kupewa fursa zaidi katika soko ambalo halina masharti magumu. Kama hoja hii ikitekelezwa vema ni wazi nchi hizi zitamudu ushindani katika biashara za ndani na zile za kimataifa. Hali iliyopo sasa haitoi fursa hizo,” alisema.
“Ili nchi masikini zimudu kuondoka katika kundi hili ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo, jukumu lililo mbele yetu ni moja ambalo ni kuweka mikakati ya wazi na kila upande kutimiza wajibu wake kama ambavyo Tanzania
imedhamiria kufanya.”
Dk. Bilal yuko jijini Instabul akiongoza ujumbe wa Tanzania unaohusisha pia wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia sambamba na wafanyabiashara.