MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal ameongoza wana-CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam katika sherehe za kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika jana kote nchini.
Katika sherehe hizo zilizofanyika katika viwanja vya Kituo cha Mabasi Kibada maeneo ya Kigamboni Dk. Bilal aliwataka wana-CCM nchini kuendelea kujenga imani na chama chao kwa kuwa kimeongoza kwa miaka 37 kwa amani na utulivu na kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi.
Makamu wa Rais ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alisema pamoja na changamoto zinazojitokeza Chama hicho kimeendelea kudumisha amani na kuimarisha demokrasia nchini.
“Tunakerana…lakini hatukamatani mashati, hatupigani mapanga. Wako wachache wanaandamana lakini CCM kimetulia na kuendelea kudumisha amani na utulivu,” alisema Dk. Bilal.
Akizungumzia kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Makamu wa Rais aliwaambia wananchi hao kuwa muungano wa serikali mbili unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili za muungano.
Akijibu malalamiko ya wananchi wa Kigamboni kuhusu kuchelewa kutolewa kwa fidia ya nyumba zao kufuatia mpango wa serikali wa kujenga mji wa kisasa wa Kigamboni Dk. Bilal alisema atamwagiza Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi akutane na wananchi hao na kuwajulisha hatua iliyofikia katika kuwalipa fidia zao.
Makamu wa Rais ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Dar es salaam, alisema mpango wa kujenga mji wa kisasa wa Kigamboni ni mradi mkubwa ambao utatekelezwa na serikali na kusisitiza ni muhimu wananchi washirikishwe hatua kwa hatua katika suala zima la kuwapatia fidia zao.