Na Mwandishi Maalumu
Ofisi ya Makamu wa Rais
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kufanya mazungumzo na Chama cha Wakala wa Forodha nchini ili kuondoa mvutano uliopo na
hivyo kuimarisha ufanisi katika shughuli za kutoa mizigo bandarini.
Dk. Bilal ameyasema hayo jana kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na Mwenyekiti wa
chama hicho, Otieno Igogo wakati alipofanya ziara fupi kukagua na kuona shughuli
zinazofanywa na Bandari ya Dar es salaam.
Akijibu malalamiko hayo Dk. Bilal alisema kuwa Serikali ingependa kuona kila mdau wa bandari
anatimiza wajibu wake kwa uwazi na mapato ya eneo hilo yanaongezeka kutokana na kufanya kazi
kwa ufanisi.
Awali, akiwasilisha malalamiko hayo, Igogo aliitaka Serikali kuchukua hatua kuhakikisha
inaondoa urasimu unasababisha ucheleweshwaji wa utoaji mizigo bandarini kiasi cha kuwafanya
baadhi ya waagizaji kutumia bandari zingine kama ya Mombasa kwa kupitisha mizigo yao.
Igogo alimweleza Makamu wa rais kuwa Idara ya Forodha chini ya TRA haiwapi nafasi mawakala
hao kuwasiliana na uongozi ili kutatua matatizo yao yakiwemo ya kucheleweshwa kwa taratibu
za kutoa mizigo, kutozwa malipo ambayo wanadai hayastahili.
Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa TRA Hurry Kitilya alimweleza Makamu wa Rais kuwa ofisi yake iko
tayari kufanya mazungumzo na mawakala hao Jumatatu ijayo.
Wadau wengine wa bandari waliokuwepo kwenye ziara hiyo waliiomba serikali kupanua
miundombinu ya upokeaji wa mafuta ili kupunguza msongamano wa malori ya kubeba mafuta na
iharakishe kuiunganisha bandari na njia nyingine za mawasiliano hasa reli ili kuongeza
ufanisi.
Akifafanua Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Meli nchini, Emmanuel Malya alieleza kuwa
kutokana na kukwama kwa usafiri wa reli, ufanisi wa bandari, umepungua kufuatia mizigo
kusafirishwa kwa magari ambayo hayawezi kuchukua mizigo mingi jambo ambalo linasababisha
waagizaji kukimbilia bandari nyingine za nchi jirani.
Akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais, Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Emphraim
Mgawe alieleza changamoto zinazoikabali bandari hiyo kuwa ni pamoja na ongezeko la shehena
ambapo juhudi zimefanywa kupanua maeneo ndani ya bandari, kushindwa kwa meli kubwa kutia
nanga kutokana na kina kifupi cha maji ya bahari.
Changamoto nyingine ni kuongezeka kwa meli katika bandari hiyo kutoka nje na ushindani
uliopo na bandari za Mombasa, Afrika KusininaMsumbiji. Katika ziara hiyo Dk. Bilal
alitembelea mlango namba 7 ambako ni kituo cha kupakulia mizigo mchanganyiko, kituo cha
kupakulia mafuta na kwenye maeneo ya kontena.