MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Uongozi wa Kampuni ya NEC yenye makao yake makuu jijini Tokyo nchini Japan. Ujumbe wa NEC – Japan umeongozwa na Rais wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na masuala ya Mawasiliano na Teknolojia, Dk. Nobuhiro Endo.
Ujio wa Kampuni hii nchini Tanzania unatokana na mwaliko wa Tanzania kwa makampuni ya Japan kufuatia ziara ya kikazi aliyoifanya Makamu wa Rais nchini Japan, mwezi wa Mei mwaka huu. Mheshimiwa Makamu wa Rais alitembelea Makao Makuu ya Kampuni hiyo wakati za ziara hiyo.
Katika mazungumzo na uongozi wa NEC Makamu wa Rais aliwaeleza wageni wake nia ya Tanzania kuona inatanua mawasiliano na teknolojia nchini ili kuinua uchumi na akafafanua kuwa teknolojia yoyote kutoka NEC inakaribishwa hapa nchini ili kusaidia Tanzania kupiga hatua.
Uongozi wa NEC nao ulimueleza Makamu wa Rais kuwa, NEC inaushirikiano wa karibu na Shirika la Simu Tanzania (TTCL) na kwamba wanatarajia kukutana na uongozi wa wizara ya Mambo ya Ndani kwa lengo la kutazama fursa za kusaidia teknolojia katika ulinzi.