MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, Julai 06, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Malawi, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Civo jijini Lilongwe. Katika sherehe hizo pamoja na Makamu wa Rais wa Tanzania, pia alihudhuria Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Waziri Mkuu wa Msumbiji na viongozi mbalimbali waliowakilisha nchi kutoka Afrika.
Sherehe hizo zilianza kwa ibada ya misa asubuhi na kisha kuhamia katika uwanja wa Civo mchana ambapo Rais wa Malawi Prof. Athur Peter Mutharika alikagua gwaride na kisha kuwasha Mwenye wa Jubilee ya miaka 50 na baadaye kulihutubia taifa.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Mutharika alisisitiza kuhusu umuhimu wananchi wa Malawi kuwa wamoja na akaeleza nia yake ya kujenga umoja kwa nchi zinazoizunguka Malawi pamoja na zile za Kusini mwa Afrika. Baada ya hotuba hiyo, sherehe hizo ziliendelea na mchezo wa soka baina ya timu ya taifa ya Malawi na Msumbiji.
Malawi ilipata uhuru wake mwaka 1984 ikiongozwa na Rais wake wa kwanza Dk. Kamuzu Banda hadi mwaka 1994. Baada ya mwaka huo alifuata Rais Dk. Bakili Muluzi aliyetawala kuanzia mwaka 1994 hadi 2004.
Baaada ya mwaka huo alifuata Rais Profesa Bingu wa Mutharika aliyetawala hadi mauti yalipomkuta mwaka 2012. Dk. Joyce Banda aliyekuwa Makamu wa Rais wa Mutharika alichukua madaraka na kukaa hadi mwaka huu 2014 ambapo Malawi iliingia katika uchaguzi mkuu na kisha Rais Profesa Arthur Peter Mutharika aliposhinda uchaguzi huo na hivyo kuwa Rais wa nne wa Malawi.
Katika sherehe hizo Makamu wa Rais pia alifuatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Mheshimiwa Makamu wa Rais amerejea nyumbani Tanzania Julai 07, 2014 tayari kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.