Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
NAIBU Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha Rose Migiro ametoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit hivi karibuni.
Dk. Migiro alitoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar, wananchi wa Zanzibar, Watanzania na wageni wote waliopata janga hilo na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua juhudi kubwa za kukabiliana na janga hilo pamoja na mikakati madhubuti iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa siku za usoni.
Katika ziara hiyo ambayo, Dk. Migiro amepongeza juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo aliambatana na baadhi ya viongozi wengine wa UN kutoka Tanzania.
Katika mazungumzo yake Naibu Katibu huyo mstaafu wa UN, alisema kuwa ujio wake ni kwa ajili ya kutoa pole kwa misiba yote miwili ya kuzama kwa meli iliyotokea nchini ndani ya kipindi kifupi. Mbali ya hayo Dk. Migiro alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi wa Zanzibar kwa mashirikiano makubwa waliyompa katika utendaji wake wa kazi kwa kipindi chote cha miaka mitano na nusu.
Dk. Migiro alieleza kuwa miongoni mwa sifa ambazo zimeweza kujenga jina zuri la Zanzibar pamoja na Tanzania nzima kwa ujumla ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kupata sifa ni pale Serikali ya Zanzibar kuziweka afisi za Umoja wa Mataifa zinazofanya kazi zake hapa nchini katika jengo moja “ONE UN”liliopo Kinazini mjini Unguja.
“Kwa kweli hatua ile imenijengea sifa kubwa kwani ni kitu ambacho kimekuwa kikisisitizwa na Umoja wa Mataifa sasa kwa upande wa Zanzibar kufanya hivyo, kwa kweli ni sifa kubwa na hata Katibu mwenyewe mkuu wa UN ameliona hilo na anatoa pongezi zake kwa mara nyengine tena,” alisema Dk. Migiro.
Naye Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. AliMohamed Shein alitoa shukurani kwa ujio wa Naibu Katibu huyo Mstaafu wa UN hapa Zanzibar ukiwa na lengo la kutoa mkono wa pole kufuatia tukio hilo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Dk. Migiro kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na Serikali, taasisi zake vikiwemo vikosi vya SMZ na SMT pamoja na taasisi binafsi na wananchi kwa ujumla katika kupambana na janga hilo la kitaifa.
Dk. Shein alieleza kuwa juhudi kubwa zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kujenga uwezo wa kuhakikisha kuwa meli zote zinazotumika kuwasafirisha wananchi ziko salama huku akieleza kuwa Jumuiya na nchi kadhaa zimeahidi kuunga mkono juhudi hizo za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pamoja na hayo Dk. Shein alieleza kuwa tukio hilo ni kubwa na limehuzunisha sana ambalo pia limeweza kujenga uimarisho juu ya hatua hizo za Serikali.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda alifika ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kutoa mkono wake wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyewekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kufuatia ajili hiyo ya meli.
Katika maelezo yake Waziri Mkuu Pinda alitoa mkono wake wa pole kwa yote yaliotokea na kusisitiza kuwa mashirikiano zaidi yanahitajika kwa Mamlaka za Usafiri wa Bahari hapa nchini.
Naye Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa Waziri Mkuu Pinda kwa ujio wake huo na kupongeza juhudi na mashirikiano iliyoyatoa Afisi yake pamoja na viongozi akiwemo Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Spika, Wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Mauungano wa Tanzania na taasisi zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa mashirikiano ya pamoja kwa Mamlaka za usafiri wa Bahari yanahitajika hatua ambayo itasaidia kufanya kazi zaidi kwa mashirikiano.
Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi ambazo Serikali imeamua kuchukua ni kununua meli nyengine mpya ambayo itawasaidia wananchi katika suala zima la usafiri waliouzoea ambayo ambayo pia itakuwa salama zaidi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wanahistoria ya kuwa na meli za Serikali ambazo huenda sambamba katika safari zake kati ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam na kuweza kuwasaidia wananchi katika usafiri huo wa bahari pamoja na mizigo yao.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa lengo na madhumuni ni kuwasaidia wananchi na kusisitiza kuwa wawekezaji nao wana nafasi yao katika hili, hivyo Serikali haijawakataza wawekezaji kufanya biashara hii ambayo itakwenda kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa.