Diwani Chadema amshtaki Mkurugenzi wa Halmashauri

Na Mwandishi Wetu
Sumbawanga

DIWANI wa Kata ya Makanyagio wa Chama cha Demikrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani Mpanda, Iddy Nziguye amemfikisha mahakamani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda, kwa tuhuma za kutumia sheria za halmashauri ya mji huo kabla hazijapitishwa na kuthibitishwa kitaratibu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana mjini hapa na Diwani Nziguye amethibitisha kuwa amefungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mpanda na kupokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Richard Kasele.

Katika madai yake diwani huyo amedai kuwa Mkurugenzi ameruhusu kutumika kwa sheria ndogo za kuhifadhi mazingira ya Mji wa Mpanda 2011, kabla ya kutoa tangazo kwenye gazeti la Serikali kama utaratibu unavyoeleza.

Amedai sheria hizo ndogo zimekuwa zikitumika bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika kama sheria inavyoelekeza. Pia amedai majina ya baadhi ya viongozi yamekuwa yakitumika kwenye karatasi zinazoelekeza sheria hizo kinyume na taratibu.

Awali chama cha CHADEMA kilimuandikia barua Mkurugenzi wa Wilaya ya Mpanda ya machi 30 2011 yenye kumbu na. CDM /JB/MPN/270 /2011 ikimshauri na kumuomba Mkuregenzi wa mji huo asitishe matumizi ya sheria ndogo za mji huo.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda Joseph Mchina alikijibu chama hicho kupitia barua ya Aprili 11, 2011 yenye kumb. Na RK/MTC/A 50/561 na kukiri kwamba sheria ndogo zote baada ya kutungwa lazima zipitie kwa wananchi.

Hata hivyo Nzigule ameliambia gazeti hili kuwa ana vivielelezo vya ushahidi juu ya kesi hiyo ambavyo amevikusanya zikiwemo risiti mbalimbali ambazo wamelipa faini baadhi ya wakazi wa mji huo kutokana na makosa ya uvunjaji wa sheria hizo na kupewa risiti namba03675 mpaka 03680.

Naye Kaimu Mkurugenzi, Mchina akifafanua juu ya kesi hiyo amekana halmashauri yake kuanza kutumia sheria hizo ndogo isipokuwa wanatumia sheria mama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda, Enock Gwambasa amedai amesikitishwa na kitendo cha diwani huyo wa Kata ya Makanyagio kumshtaki mkurugenzi kwa madai kuwa wakati sheria hizo zinapitishwa na Baraza la Madiwani Diwani huyo pia alikuwemo kwenye kikao hicho.