DIT wavumbua ‘mbadala’ wa mgawo wa umeme


Mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Noel Ngomo akitoa maelezo namna kifaa hicho kinachotunza umeme kinavyofanya kazi.

Na Joachim Mushi

TAASISI ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) imebuni kifaa kinachoweza kuifadhi umeme na kutumika pale umeme unapokatika, huku kikiwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kujiongoza chenyewe.

Kifaa hicho chenye uwezo wa kuifadhi umeme wenye nguvu za watts 3,000 kimetengenezwa na baadhi ya wanafunzi wa DIT kutoka vitengo mbalimbali vya ufundi na kinauwezo wa kuifadhi umeme unaotokana na vyanzo anuai vya nguvu za umeme.

Akizungumza na matandao wa dev.kisakuzi.com kwenye maonesho ya 35 ya Biashara ya Kimataifa mmoja wa wanafunzi waliotengeneza kifaa hicho, Noel Ngomo alisema mfumo huo unaweza kuwa msaada mkubwa wa wananchi hasa kipindi hiki cha mgawo wa umeme nchi nzima.

Ngomo alisema mfumo wa kifaa hicho unapofungwa nyumbani unauwezo wa kuhifadhi umeme watts 3,000 na kutumika moja kwa moja pale umeme unapokatika, bila mtumiaji kujua kama umeme umekatika.

“Kifaa hiki kinapofungwa ndani huwa kinahifadhi umeme pale unapokuwepo wa kawaida na baada ya kukatika chenyewe kinajiunganisha na kuanza kutoa umeme moja kwa moja, hivyo mtumiaji hawezi kujua kama umeme wa kawaida umekatika,” alisema Ngomo.

Aidha alisema kifaa hicho kimetengenezwa kutumika maeneo yote, vijijini na hata mjini. Kwa vijijini kinaweza kuunganishwa na umeme wa nguvu za jua au ule wa upepo, lakini mjini kinafungwa na mfumo wa umeme wa kawaida.

“Kinauwezo wa kuendesha friji, televisheni, taa, feni, radio, pasi ya umeme, pampu za maji na vifaa vingine vya kawaida vya umeme…na bei yake inafikia sh. milioni 1.8 hadi mbili kulingana na uwezo wa mfumo,” alisema Ngomo.