MSANII nyota wa muziki wa bongo fleva Nasib Abdul a.k.a Diamond Platnumz amesema kamwe hawezi kwenda mahakamani kumshtaki mtu kwa ajili ya kashfa na vituko ambavyo vimekuwa vikimuandama kwenye vyombo vya habari. Msanii huyo Diamond Platnumz alisema kwa sasa yeye ni msanii pekee ambaye anaandikwa sana na vyombo vya habari kuhusiana na kasha na maswala mengine katika maisha yake binafsi lakini kamwe hawezi kwenda kulalamika mahakamani kwa kuwa anajua nini anachokifanya.
Diamond ametoa kauli hiyo usiku wakuamkia leo alipokuwa akifanya mahojiano na kipindi cha Friday Night Live (FNL), kinachorushwa na kituo cha televisheni ya Channel 5 (EATV) cha jijini Dar es Salaam. Akizungumza katika kipindi hicho Diamond alisema licha ya kwamba yeye kwa sasa ni msanii pekee anayeongoza kwa kuandikwa vibaya na vyombo vya habari nchini lakini kamwe hawezi kwenda mahakamani kulalamikia kitendo hicho.
Aidha alisema anachoangalia yeye ni namna gani anaweza kufanya vizuri katika kazi yake ya usanii lakini sio kulalamika mahakamani na namna ambavyo anaandikwa vibaya na vyombo vya habari.
“…Kwa kusema kweli mimi ni mwanamuziki pekee ambaye naongoza kwa kuandikwa vibaya na vyombo vya habari lakini kamwe siwezi kwenda mahakamani kulalamikia kitendo hicho maana binafsi najua nini ninachokifanya katika muziki,” alisema Diamond akihojiwa na chombo hicho cha habari.
Aidha katika hatua nyingine mwanamuziki huyo nyota nchini alisema anatarajia kufanya show ya kufa mtu katika siku ya msanii katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salam (Jumamosi) hivyo kuwataka wananchi kuja kwa wingi katika onesho hilo.
Alisema katika show hiyo anatarajia kufanya show ya heshima kwa watu wa makamu hivyo kuomba wazazi kumiminika kwa wingi kwenye show hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam. “…Kimsingi Show hiyo itakuwa ya heshima na kali kwa watu wazima…hata mama yangu mzazi atakuwepo naomba mashabiki waje kuona burudani ya kufa mtu hiyo siku…,” alisema Diamondi katika mahojiano hayo.