Na Mwandishi Wetu,
MSANII wa Muziki wa Kizazi kipya Naseeb Abdullah a.k.a Diamond Platinamz amezidi kujichanganya katika kosa linalomkabili na kutumia mavazi wa JWTZ kwenye show yake aliyoifanya katika Tamasha la Fiesta lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Vichekesho zaidi vya msanii huyo maarufu amevifanya pale alipoamua kuandika barua ya kuliomba radhi Jeshi la Wananchi Tanzania kwa kitendo cha kutumia mavazi yao kinyume na sheria. Kwa mujibu wa barua inayodaiwa kuandikwa na Diamond toka katika kampuni anayofanya nayo kazi ya Wasafi Classic Baby Co. (WCB) msanii huyo amejichanganya kwa kuliandikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akiliomba radhi huku yeye akidhani ndio Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Barua hiyo inayoonesha vituko zaidi vya msanii huyo imeandikwa tena ikiwa haikuzingatia taratibu za uandishi wa barua za kiofisi huku ikiwa na makosa kedekede ya kiuandishi kimaneno jambo ambalo mtu akiisoma inaonesha mzaha ukilinganisha na kosa linalomkabili.
Mfano anuani ya Jeshi ameiandika; The United Republic of Tanzania, Jeshi la Kujenga Taifa (JWTZ), Makao Makuu Dar es Salaam Tanzania, pia akaanza na neno Dear… Hata hivyo katika barua hiyo Diamond amekiri kosa la kutumia mavazi alisi ya JWTZ bila ya idhini huku akiliomba jeshi hilo limsamehe kwa kitendo hicho. Kituko zaidi ni kwamba barua hiyo ameiandika kwenda JKT huku yeye akiamini ndio JWTZ jambo ambalo linazidisha utata na mzaha kwa kitendo alichokifanya. Barua halisi inayondaiwa kuandikwa na Diamond imeambatanishwa na habari hii.