Na Mwandishi Wetu, Dar
MSANII wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul a.k.a Diamond Platinum usiku huu jijini Dar es Salaam amefanya kufuru baada ya kunyakua tuzo zote za vipengele tofauti alivyoshindanishwa kwenye Shindano la Tuzo za Muziki, maarufu kama ‘Kilimanjaro Tanzania Music Award’ (KTMA).
Diamond alitwaa tuzo zote saba alizoshiriki kushindanishwa na kuweka historia katika mashindano hayo. Katika shindano hilo Diamond alikuwa akishindania tuzo za Wimbo Bora wa Pop, Mwimbaji Bora wa Kiume wa Kizazi Kipya, Msanii Bora wa Kushirikishwa/Kushirikiana, Mtunzi Bora wa Mwaka wa Kikazi Kipya, Video Bora ya Mwaka, Wimbo Bora wa Mwaka na Mtumbuizaji Bora wa Kiume.
Katika vipengele hivyo Diamond alifanikiwa kutwaa tuzo zote saba na kuwabwaga washindani wake. Katika hafla hiyo moja ya tuzo hizo alikabidhiwa na mpenzi wake, Wema Sepetu ambaye alionekana kufuraishwa zaidi na mafanikio wa rafiki yake huyo ambaye amerudiana kimapenzi hivi karibuni.
Mara zote Diamond alipopanda jukwaani kuchukua tuzo zake hakuacha kumtaja kwa kumshukuru mpenzi wake Wema Sepetu.
Baadhi ya wasanii wengine waliopata tuzo nyingi ni pamoja na Mzee Yusuf a.k.a Mfalme mwimbaji wa nyimbo za taarab kutoka kundi la Jahazi Modern Taarab ambaye alishinda tuzo nne moja ikiwa ni ya bendi yake, Judith Wambura a.k.a Lady Jay Dee ambaye alijinyakulia tuzo mbili, Isha Mashauzi ambaye amepata tuzo mbili, Fid Q tuzo mbili, Mashujaa Bandi ambao walijinyakulia tuzo mbili.
Wasanii wengine walioshinda tuzo moja moja ni pamoja na Young Killer, Chibwa, Double Do, Lwiza Mbutu, Jose Mara, Ferguson, Weusi, Vanesa Mdee, Niki wa II, Ney wa Mitego, Jose Chamilion, Christiani Bella, Enrico, Amoroso, Man Water, Hassan Bichuka na Masood Masood.
Tuzo hizo za Kilimanjaro Tanzania Music Award zilipambwa na burudani za wasanii mbalimbali wa ndani ya nchi.