Dewji amwaga mahindi tani 100 kwa wapigakura wake

Na Mwandishi Wetu
Singida

MBUNGE wa Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mohammed Dewji, ametoa msaada wa tani 100 za mahindi zenye thamani ya sh. milioni 40 kwa wananchi wa vijiji 20, wanaokabiliwa na upungufu wa chakula kwenye jimbo hilo.

Akizungumza jana katika hafla fupi ya kukabidhi msaada huo, Dewji alisema amefikia uamuzi huo wa kutoa msaada kwa familia zinazokabiliwa na njaa, baada ya kupewa taarifa ya tatizo hilo na madiwani wa kata zilizoko maeneo ya vijijini.

Dewji maarufu kwa jina la (MO) ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kutoka Mkoa wa Singida alisema anatambua wazi kwamba mahindi hayo anayoyasambaza hivi sasa, hayatakidhi mahitaji ya familia husika bali kupunguza ukubwa wa tatizo.

“Lakini hata hivyo, imani yangu ni kwamba msaada huu, utapunguza sana makali ya uhaba wa chakula unaozikabili familia nyingi za vijijini,” alisema.

Aidha aliongeza kuwa yeye kama mbunge wa wananchi wanaokabiliwa na upungufu wa chakula na pamoja na Serikali, hawatakubali kuona wananchi hao wanapata usumbufu wa aina yoyote ikiwemo kufa kwa njaa.

“Ndugu zangu wananchi, leo nimewatangulizia chakula hichi, lakini kama mbunge wenu, nitaendelea na jitihada za kuiomba Serikali yetu itupatie chakula cha bei nafuu ili kiweze kukidhi mahitaji yetu,” alisisitiza MO.

Aidha alitumia fursa hiyo kutoa tahadhari kwa viongozi watakaoshiriki kugawa mahindi hayo, kuwa waadilifu na wafuate vigezo zilivyowekwa ili walengwa wote wapate msaada huo bila kupunjwa na kwa wakati.

Pamoja na hayo aliwataka wananchi wanaokabiliwa na upungufu wa chakula wasikate tamaa kutokana na matatizo haya ya kukabiliwa na upungufu wa chakula kuendelea kupokea ushauri wa wataalamu msimu ujao.

“Utakapofika wakati wa kuandaa kilimo katika msimu ujao, tuwatumie wataalam wetu vizuri ili tuweze kulima kwa kufuata maelekeo ya kitaalam. Hapo naamini kuwa tutafanikiwa na kupata mazao yanayostahili na yenye tija,” alisema.

MWISHO.