Denmark Yaifagilia Tanzania kwa Utajiri Kiutamaduni…!

Balozi wa Denmark nchini Tanzania,Bw. Johnny Flentoe akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa program mpya ya CKU.

Balozi wa Denmark nchini Tanzania,Bw. Johnny Flentoe akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa program mpya ya CKU.

 
KWA mujibu wa Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Johnny Flentoe, amesema kwamba Tanzania inautajiri mkubwa wa kiutamaduni ambao unaweza kutumiwa kuchangia pato la taifa GDP.
 “Bado tasnia ya sanaa na ubunifu ambayo ingeliweza kuchangia katika uchumi na kuwapatia kazi vijana haijatumika ipasavyo. Kutokana na hilo kipaumbele cha programu hii mpya ni kuwezesha vijana kutumia sanaa na ubunifu kukuza ajira,” anasema balozi Johnny Flentoe.
Mshairi Jasper Sabuni akifanya kazi ya ‘spoken words’ wakati wa uzinduzi wa program mpya ya CKU.
Juni 5, 2015, Ubalozi wa Denmark ukishirikiana na Kituo cha Utamaduni na Maendeleo cha Denmark (CKU) umezindua program mpya ya utamaduni na  maendeleo Tanzania ( Tanzania Culture and Development Programme).
Programu hiyo imelenga kutengeneza fursa za kiuchumi kupitia jukwaa la sanaa na ubunifu ambapo watanzania watajipambanua kupitia kushiriki shughuli mbalimbali za kitamaduni na kujipatia kipato.
Baadhi ya wadau waliofika kwenye uzinduzi wa program mpya ya CKU Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja
CKU inatekeleza program hiyo kupitia kwa washirika wake likwemo Tamasha la
Kimataifa la Filamu
(Zanzibar International Film Festival (ZIFF), kupitia mradi wao
wa Village Panorama ambao unalenga kuonyesha filamu za kuelimisha maeneo ya vijijini
huko Zanzibar.
Taasisi nyingine ni Culture and Development in East Africa (CDEA), ambao watafanya utafiti wa namba sanaa ya muziki na filamu inavyochangia katika pato la taifa, wakati taasisi ya Soma Book Café ikiindesha mashindano ya uandishi na usomaji wa vitabu.
Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) wao watanufaika na program hiyo kwa kupatiwa vifaa vya muziki vya kufundishia huku Nafasi Art Space ambacho ni kituo cha sanaa kikiboreshwa na kupata uwezo wa kutumika kama kituo kikubwa cha sanaa za maonesho.  
Meneja wa CKU Afrika Mashariki, Christoph Lodemann akitoa maelezo mafupi juu ya program mpya ya Tanzania
“Sanaa ina uwezo mkubwa wa kuwezesha majadiliano na kupaza sauti ya umma. Ndio maana Denmark inawezesha kuwapo kwa jukwaa ili wananchi waweze kujieleza wenyewe kupitia sanaa. Kwa kukuza vipaji vya wasanii wapya nchini Tanzania, Denmark inatoa mchango wake mkubwa kwa wasanii na wabunifu,”  anasema meneja wa CKU Afrika Mashariki Christoph Lodemann.
Denmark inawezesha shughuli za sanaa, utamaduni  na ubunifu wa kisanii nchini
Tanzania kama mchango wake katika juhudi za kukuza uchumi wa taifa hili.