Demokrasia Hutegemea Uwepo wa Vyombo vya Habari – TAMWA

Washiriki katika mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi Mkuu 2015 uliofanyika mjini Arusha.

Washiriki katika mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi Mkuu 2015 uliofanyika mjini Arusha.

 

IMEELEZWA kuwa vyombo vya habari ni daraja muhimu kwa uwepo wa demokrasia kwenye uchaguzi wowote. Na demokrasia haiwezi kuwepo pasipo vyombo vya habari. Hii ni kwa sababu uchaguzi huru na wa haki siyo tu kuhusisha uhuru wa kupiga kura lakini pia utoaji wa elimu ya jinsi kwa wapiga kura, kuhusu mchakato shirikishi ambapo wapiga kura hushiriki katika mijadala ya umma na kupata taarifa za kutosha kuhusu vyama, sera, wagombea na michakato ya uchaguzi yenyewe ili kufanya maamuzi sahihi.

Hayo yamebainishwa na Afisa Miradi wa TAMWA, Edson Sosten wakati wa uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi Mkuu 2015 hiyo iliyowasilishwa na TAMWA mjini Arusha.

“Kwa mujibu wa ripoti ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi Mkuu 2015 iliyototolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ilibainisha kuwa vyombo vya habari viliwafikia wanawake kwa asilimia 10% tu”. alisema Sosten.

Akifafanua aliongeza kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika Mwaka 2015 ulionyesha kuwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu walikosa nafasi kwenye vyombo vya habari. Kama ilivyokuwa mwaka 2005 na 2010 wakati wa uchaguzi. Vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 viliendelea kuripoti zaidi habari za wagombea wanaume iwe ni kwa kuwatumia kama vyanzo vikuu vya habari au kwa namna yoyote yenye kutoa wigo mpana wa wanaume kusikika zaudi katika jamii.

Matokeo ya tathimi hiyo ya jinsi gani vyombo vya habari viliripoti habari zinazohusu wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yamebaini kuwa wanaume wanaongoza katika makundi yote ya mada za habari hata kwenye zile habari ambazo zilikuwa hazihusiani na Uchaguzi, pamoja na nyingine kama vile uhalifu, nishati na serikali. Aidha ilikuwa ni nadra sana kupata vyanzo vya habari vilivyowahusisha wanawake katika kurasa za mbele za magazeti. Wengi wao huanza kuonekana baada ya ukurasa wa nne wa gazeti.

 

Washiriki katika mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi Mkuu 2015 uliofanyika mjini Arusha.

Washiriki katika mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi Mkuu 2015 uliofanyika mjini Arusha.

 

Vyombo vya habari vilivyofanyiwa tathimini ni;magazeti mawaili yanayomilikiwa na Serikali ( Daily News na Habari Leo) na magazeti mawili binafsi (Nipashe na Mwananchi); Runinga (TV channel) inayomilikiwa na Serikali (TBC1) Kituo cha runinga binafsi kimoja (Azam TV) na chombo cha mwisho ni kituo cha redio ya serikali (TBC Taifa) .

Kwa mujibu wa matokeo ya ufuatiliaji wa habari za magazeti, redio na runinga, Wanawake kwa ujumla waliogombea na wasiogombea kote nchini walikabiliwa na unyanyasaji kama vile kufanyiwa ghasia, na vitisho wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi. Pia wanaume walificha kadi za kupigia kura za wake zao, wanaume waliwalazimisha wake zao kuwapigia kura wagombea ambao wanawataka hata kama mwanamke hamtaki, utumiaji wa lugha ya matusi dhidi ya wagombea wanawake na wakati wa kampeni kuna baadhi ya wagombea wanawake walikamatwa na kutishiwa kwa tuhuma za kutotii amri ya Jeshi la polisi.

Takwimu zinaonyesha wakati Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2015, wanawake waliojiandikisha kupiga kura ni 53% .Wanawake waliogombea urais walikuwa 8 lakini ni moja tu aliebakia katika hatua ya mwisho. Kwa ujumla, kulikuwa na wagombea 1,230 kwenye viti vya ubunge nchini Tanzania amabapo wanawake walikuwa 238 au 19% tu. Kati ya hawa 9% walikuwa kutoka CCM, 6% Chadema, 15% ACT Wazalendo, 11% CUF, iliyobakia ilitoka katika vyama vingine vyote vya siasa.

Kati ya wanawake 238 waligombea ubunge ni wanawake 24 sawa na 10.4% waliochaguliwa. Kwa wagombea udiwani, kulikuwa na wagombea 10,879 ambapo wanawake walikuwa 679 (6.2%) tu. Madhara ya kukosekana kwa usawa kwenye vyombo vya habari ilichagia sana takwimu tajwa hapo kushindwa kupanda badala yake wanawake wanazadi kukosa uwakilishi katika ngazi mbalimbali za maamuzi.