DC Serengeti akemea matapeli wa safari za Loliondo

Na Mwandishi Wetu
Serengeti

SERIKALI wilayani Serengeti mkoani Mara, imekilalamikia kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara kuendelea kutumia malori kusafirisha wagonjwa kwenda Loliondo kupata tiba kwa ‘Babu”, kwani kimekuwa kikileta usumbufu baada ya wagonjwa kuzuiwa na vyombo vya dora.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Edward ole Lenga, alisema kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakipakia watu kwenye malori na kupita njia za panya kwa lengo la kuwapeleka Loliondo, lakini wamekuwa wakizuia wanapofika kwenye vizuizi.

Lenga alisema kitendo hicho kimekuwa kikileta usumbufu mkubwa kwani wafanyabiashara wamekuwa wakiwatelekeza wagonjwa wakiwemo wenye hali mbaya pamoja na watoto, katika maeneo mbalimbali na wao kutokomea kusikojulikana ilhali wamelipwa nauli.

Alisema tayari malori matano kutoka maeneo ya wilaya za Meatu, Bariadi, Magu na Rorya, yaliozuiliwa hivi karibuni yametelekeza wagonjwa ambao walikuwa wakisafiri na magari hayo na wahusika kutokomea kusiko julikana.

Kufuatia hali hiyo mkuu huyo wa wilaya, amewataka wananchi
kujiepusha na wafanyabiashara wanaotumia usafiri wa malori kwani hayawezi kuruhusiwa kwenda Loliondo na badala yake watafute usafiri wa mabasi au magari madogo.

“Tunawaomba wananchi wasikubali kutapeliwa kwani malori hayaruhusiwi, Serikali ilishapiga marufuku kubeba watu kwenye malori…wananchi wasikubali kabisa, wanatapeliwa kwani watakapofika kwenye vizuizi watatelekezwa na wagonjwa wao na wahusika kutokomea kusikojulikana,” alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu wilayani Serengeti, Samwel Mewama, ameitaka Serikali wilayani humo, kuendelea na utaratibu wa kuruhusu watu kwenda Loliondo, badala ya kuwazuia ili kupunguza msongamano ulioko katika kituo cha kanda ya ziwa wilayani Bunda.

Mewama alisema kuwa kwa sasa kuna msongamano mkubwa wa watu wakiwemo wazee na watoto katika kituo kilichotengwa kwenye uwanja wa Mbuzi mjini Mugumu, ambapo baadhi yao wamefanya makazi ya muda ya kupika na kulala katika kituo hicho.

Alisema kuwa tatizo la kituo cha Bunda ni kubw, lakini kusitisha safari kituo cha Mugumu ya watu kwenda Loliondo, ni kutaka kuhamishia tatizo la kituo cha Bunda kuja Mugumu, na hivyo kuwavunjia wananchi hao haki za binadamu.

Hata hivyo alipendekeza njia pekee ya kuondoa changamoto hizo, ni kuruhusu idadi kubwa ya magari kutoka Bunda, hivyo kuzuia watu wanaotokea katika kituo cha Mugumu kwa sababu kufanya hivyo ni kuongeza tatizo jingine zaidi.