DC Handeni Awataka Wananchi Kutumia Tamasha la Utamaduni Kutafuta Fursa

Mkuu wa Wilaya Handeni, mkoani Tanga, Muhingo Rweyemamu, pichani.

Mkuu wa Wilaya Handeni, mkoani Tanga, Muhingo Rweyemamu, pichani.

Na Mwandishi Wetu, Handeni

MKUU wa wilaya Handeni, DC Muhingo Rweyemamu, amewataka wananchi wa Handeni, mkoani Tanga kulitumia Tamasha la Handeni kwa ajili ya kutafuta fursa za kimaendeleo. Akizungumza jana mjini Handeni, Muhingo alisema kutokana na tamasha hilo kufanyika mwisho wa mwaka, Desemba 14, itakuwa chachu ya kuwaunganisha watu wote, sanjari na kujadili changamoto zinazoikabiri Handeni na Tanzania kwa ujumla.

Muhingo alisema kuwa tamasha hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na kuandaliwa maalum kwa ajili ya Watanzania kwa ajili ya kuangalia ngoma na matukio mbalimbali ya kijamii.

“Wakati napongeza kwa dhati kuandaliwa kwa tamasha hili wilayani hapa, pia nawaomba watu waje kwa wingi kushuhudia namna gani Handeni imepiga hatua kimaendeleo na kuangalia namna gani wanaweza kusonga mbele.

“Naamini tutafikia hatua nzuri kwa kushirikiana na wadau wote, hivyo wale wanaoishi mbali na Handeni pia ni wakati wao kurudi nyumbani mwishoni mwa mwaka kujifunza mambo ya utamaduni wao, sanjari na kufanya juhudi za kupiga hatua kimaendeleo,” alisema.

Tamasha hilo linaloandaliwa na Mratibu wake Kambi Mbwana, hadi sasa limedhamiwa na Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.

Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, na Taifa Letu.com, huku likipangwa kuanza saa 2 za asubuhi hadi saa 12 za jioni.