DC Bunda amuweka Ofisa Afya rumande

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe

Na Shomari Binda, wa Binda News-Bunda

MKUU wa Wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe amechukua maamuzi ya kumuweka rumande Ofisa Afya wa Mji mdogo wa Kibara James Manaji kwa kile alichokieleza kushindwa kusimamia shughuli za Afya katika Mji huo na kupelekea kuonekana usiofaa kwa makazi ya Binadamu.

Akizungumza na BINDA NEWS Mkuu huyo wa Wilaya alisema Afisa huyo ameshindwa kutelekeza majukumu yake ya kazi kwa kushindwa kusimamia shughuli zake na kupelekea kuonekana Mji mchafu huku akiendelea kuchukua mshahara wa Serikali pasipo kufanya kazi zilizopo mbele yake.

Alisema makazi ya Wananchi wengi katika Mji huo zinaishi bila ya kuwa na vyoo hivyo kujisaidia ovyo na kuhatarisha Afya na hivyo huenda kupelekea kuibua kwa magonjwa na mlipuko ambayo yataatarisha maisha ya Binadamu.

Mirumbe alisema Afisa huyo ameshindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo katika masuala ya Afya kwa kusema suala la choo ni muhimu katika makazi na tayari yalishatolewa maagizo muda mrefu kwa Maafisa wote wa Afya kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo kwa ajili ya kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.

“Ni kweli nimemuweka ndani Afisa Afya wa Mji mdogo wa Kibara kwa kushindwa kusimamia majukumu yake na suala hili ni nyeti kwa sababu hakuna jambo muhimu kama kuzingatia taratibu za Afya hususani kuwa na choo katika makazi kwa sababu tulishatoa maelekezo.

“Na hili si kwa kibara tu,nimeshatoa maelekezo katika maafisa watendaji wote wa vijiji kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo na kuhakikisha mazingira ya usafi yanasimamiwa vizuri ili Wilaya ya Bunda ionekane ipo katika mazingira ya usafi kwa wakati wote,”alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Alisema suala la uwajibikaji kwa watumishi wa idara zote lazima lizingatiwe na kudai kuwa ataendelea kufanya ufatiliaji bila kikomo ili kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake wa kazi na kukomesha tabia ya kukaa ofisini na kupiga gumzo huku kazi zikiendelea kusimama.

DC Joshua Mirumbe alichukua maamuzi ya kumuweka ndani Afisa huyo wa Afya akiwa katika Mji huo wa Kibara wakati akikagua shughuli za maandalizi yakiwemo ya usafi kwa ajili ya kupokea mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa kuwasili Mjini Bunda agosti 18 huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikitarajiwa kuzinduliwa.

Kwa upande wake Afisa huyo wa Afya wa Kibara James Manaji akizungumza na BINDA NEWS baada ya kutoka ndani alikokaa kwa muda wa zaidi ya masaa 24 kabla ya kuamuliwa kutoka, alisema alishangazwa na maamuzi ya Mkuu huyo wa Wilaya kumuweka ndani bila ya kufanya Takwimu juu ya uhamasisishaji wa ujenzi wa vyoo.

Alisema kazi ya uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo inaendelea kufanyika vizuri katika vijiji vyote vinee vya Mji huo na hatua iliyochukuliwa na Mkuu huyo wa Wilaya haikuwa sahihi kwa kuwa hakufanya utafiti wowote juu ya jamabo hilo tangu ulipoanza utekelezaji wa kazi hiyo.

Alidai kuwa DC huyo amekuwa akichukua maamuzi mengine ambayo sio haki tangu alipoteuliwa kusimamia Wilaya hiyo kwa mujibu wa dhana ya utawala bora na kudai kuwa katika siku za vivi karibuni amekuwa akichukua maamuzi kama hayo bila kufanya utafiti na kuvunja haki za msingi za Binadamu.