DC Babati awataka wakulima kuunga mkono jitihada za watafiti wa mbegu

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi akizungumza na wakulima na watafiti wa Mradi wa utafiti mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA), katika maadhimisho ya Siku ya Wakulima Katika Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati.

 

Mratibu wa Mradi wa WEMA, na Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti Ilonga, Dk. Justin Ringo (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi (kulia) juu ya shamba la majaribio ya mbegu chotara za mahindi zinazostahimili magonjwa na ukame (WEMA), katika moja ya shamba la utafiti shirikishi lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati walipotembelea.

 

Mtafiti wa Mradi wa WEMA, Ismail Ngolinda (kulia) akimtembeza mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi (kushoto) ndani ya shamba la majaribio katika moja ya shamba la utafiti shirikishi lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati walipotembelea.

 

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi akitembelea shamba la majaribio ya mbegu chotara za mahindi zinazostahimili magonjwa na ukame (WEMA), katika moja ya shamba la utafiti shirikishi lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati walipotembelea.

 

 

Mtafiti wa Mradi wa WEMA, Ismail Ngolinda (kwa kwanza kulia) akijibu maswali ya baadhi ya wakulima ndani ya shamba la utafiti shirikishi lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati walipotembelea.

 

Mahindi ndani ya shamba la utafiti shirikishi na wakulima la Mradi wa WEMA lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati.

 

Mjumbe wa Kamati ya Mawasiliano na uratibu Mradi wa WEMA, Bw. Temu akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

 

Mratibu wa Mradi wa WEMA, na Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti Ilonga, Dk. Justin Ringo akijibu maswali ya wakulima (hawapo pichani) mara baada ya kutembelea shamba la utafiti shirikishi wa mbegu chotara za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA).

 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Cade Mshamu (wa pili kulia) akizungumza na wakulima na watafiti wa Mradi wa utafiti mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA), katika maadhimisho ya Siku ya Wakulima Katika Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati.

 

Baadhi ya wakulima na wageni anuai wakiwa katika mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Wakulima Katika Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati.

 

Mkulima akiuliza swali kwa watafiti katika mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Wakulima Katika Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini, wilayani Babati.

 

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Jackson Nkuba (kulia) kwenye hafla hiyo.

 

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Shabaan Husein (kulia) akizungumza kwenye hafla hiyo.

 

Na Joachim Mushi, Babati

MKUU wa Wilaya ya Babati, Raimond Mushi amewataka wakulima kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo wakiwemo watafiti wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame, magonjwa (WEMA) ili waweze kuendesha kilimo chenye tija na kuachana na kilimo cha kujikimu ambacho hakiwezi kuwapa maendeleo.

Alisema kilimo cha sasa kinapaswa kuendeshwa kisayansi na kufuata ushauri wa kitaalamu, ambapo ni pamoja na kutumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti kulingana na mahitaji ya maeneo ya wakulima. Mh. Mushi ametoa ushauri huo mjini Babati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakulima wilayani Babati ambapo pia alitembelea shamba la utafiti shirikishi wa mbegu za mahindi unaotekelezwa na watafiti kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia mradi wa utafiti wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA).

Alisema wakulima wakitaka kufanya kilimo cha manufaa hawana budi kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na kupendekezwa na wataalamu wa kilimo kutumika katika maeneo yao. “…Tuwe macho na mbegu tunazonunua ili tuweze kuvuna mazao ya kutosha, wakulima sasa lazima tubadilike tusiendeshe kilimo cha kujikimu tu…mkulima huwezi kuendelea kwa kufanya kilimo cha kujikimu, tunataka ulime upate chakula na ziada kisha uuze mazao kukuza uchumi wako na ubaki na akiba,” alisema Raimond Mushi.

Alisema serikali ya awamu ya nne imedhamiria kufanya uchumi wa viwanda hivyo wakulima wanakila sababu ya kufanyia kazi ushauri wa wataalamu wa kilimo ili waweze kuzalisha mazao ya kutosha yatakayotumika kama mazao ghafi kwenye viwanda na kunufaika zaidi.

“Tunapolima sasa tulime kisayansi na kwa malengo, tutumie maeneo yetu vizuri ili tuweze kuzalisha mazao ya kutosha,” alisisitiza Mkuu wa Wilaya, Raimond Mushi na kuongeza eneo la kilimo kwa sasa linapungua kutokana na ongezeko la idadi ya watu nchini hivyo kuna kila sababu ya kutumia eneo dogo linaloleta matokeo makubwa na manufaa kwa mkulima.

Alisema serikali imedhamiria kuleta mabadiliko kwa wakulima ndio maana inawawezesha wataalamu kama WEMA na kuwaunga mkono shughuli za utafiti kwa maendeleo ya wananchi hawa wakulima. “Sisi hapa Babati tunangoja kwa hamu matokeo ya utafiti ili tuweze kuyafanyia kazi…tuleteeni mapema tutasimamia na kuhamasisha wakulima wetu kutumia mbegu za WEMA,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Jackson Nkuba alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na makampuni yatakayojitokeza kuzalisha mbegu za WEMA na zingine bora zinazofanyiwa utafiti ili wakulima wazipate kirahisi, hivyo kutoa rai kujitokeza kwa wingi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Babati, Bw. Mushi, viongozi mbalimbali katika tukio hilo wakiwemo wakulima kwa pamoja walitembelea shamba la utafiti shirikishi wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA) lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini na kujionea mbegu zilizofanyiwa utafiti wa WEMA na kujionea matokeo ya utafiti.