KUIMARIKA kwa Ulinzi na Usalama katika mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mji wa Sirari mkoani Mara kumetajwa kuwa chanzo cha kuimarika kwa shughuli za biashara katika eneo hilo. Hata hivyo, uwepo wa njia nyingi zisizo rasmi na upungufu wa watumishi wa mamlaka za Serikali na vitendea kazi katika mpaka huo, umeendelea kuwa sababu inayokwamisha mpango wa Serikali wa kukomesha vitendo vya ukwepaji kodi na biashara za magendo katika eneo hilo.
Hayo ni baadhi ya mambo yaliyojiri katika ziara ya ghafla ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyalandu, alipotembelea mji wa Sirari katika mwendelezo wa ziara zake za kukagua maeneo ya mipaka ya Tanzania na nchi jirani kwa lengo la kukagua vituo vya pamoja na masoko ya mipakani.
Akimkaribisha Naibu Waziri Makao makuu ya Wilaya ya Tarime, Mkuu wa Wilaya, John Henjewele na Mbunge wa Tarime Nyambari Nyangwine wamesema, jitihada za Serikali za kuimarisha amani na utulivu katika Wilaya hiyo na Mkoa wa Mara kwa ujumla, zimeufanya Mkoa huo kuanza kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa.
“Tunaendelea kupambana na vitendo vya uhalifu kama biashara za magendo, raia kumiliki silaha kinyume cha sheria, ujambazi na uhasama wa koo za wenyeji wa eneo hili, hali hii ina mchango mkubwa katika kufanikisha shughuli za biashara hasa katika mpaka wetu wa Sirari ambao ukitumika vyema, waweweza kutoa mchango mkubwa kwa pato la Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hizo, Nyalandu amewataka wakazi wa mji huo kushiriki kikamilifu katika biashara halali na kufuata sheria ili kufaidika na fursa zilizopo katika maeneo ya mipakani.
Aidha amewataka watendaji wa serikali katika mji wa Sirari kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ili washindane na majirani zetu kwa kufika kila wanakofika na kupeleka bidhaa zenye ubora.
Kuhusu agizo la Serikali la kupiga marufuku biashara ya sukari kuvuka mipaka ya nchi, Nyalandu amesema… “Serikali imepiga marufuku biashara ya sukari kutoka nje ya mipaka yetu, sukari inayopatikana nchini ni kwa ajili ya Watanzania, imesamehewa kodi, ni marufuku kuuza nje ya nchi.”
Amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana na wananchi kudhibiti aina yoyote ya magendo katika mpaka huo na kuagiza taratibu za kisheria kuchukuliwa dhidi ya yoyote atakayekiuka kwa makusudi agizo hilo.