Loliondo
MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Ambilike Mwasapile amesema licha ya umati wa watu kuendelea kufurika nyumbani kwake ataendelea kutoa dawa hiyo kwa wagonjwa kadri wanavyokuja.
Hadi jana takribani watu zaidi ya 3,000 walikuwa wakiendelea kufurika nyumbani kwa mzee huyo anayedaiwa kuwa na dawa aliyooteshwa na Mungu ambayo inatibu magonjwa matano sugu kwa pamoja, yaani Kisukari, Ukimwi, Presha, Kansa na Pumu kwa lengo la kupata huduma ya dawa hiyo.
Ambilike Mwasapile amesema bado ataendelea kuwahudumia watu watakaofika nyumbani kwake. Pamoja na hayo amewaonya baadhi ya watu wenye magari ya usafiri ambao wamekuwa wakipandisha bei ya nauli kutokana na idadi kubwa ya watu kutaka kwenda kijijini kwake.
Akizungumza nyumbani kwake na vyombo vya habari juzi Mchungaji Mwasapile, amesema, hivi sasa zaidi ya watu 3,000 wanakwenda nyumbani kwake katika Kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro kwa ajili ya kunywa dawa kwa gharama ya Sh. 500 kama alivyoagizwa na Mungu katika ndoto.
“Watu ni wengi wanakimbilia uponyaji na hawa bado ni tone katika wale wanaondelea kuja hapa, nisingependa kuona wafanyabiashara wakianza kuwaumiza watu wanaokuja kunywa dawa.
“Hii ni agizo kutoka kwa Mungu kwamba dawa hii itolewe kwa kiwango cha Sh. 500 kwa hiyo hata wao wanapaswa kuwatoza gharama za kawaida kabisa za nauli watu wanaokuja huku,” alisema Mchungaji Mwasapila ambaye hivi sasa amejizoelea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.
Onyo la Mchungaji Mwasapile limekuja muda mfupi baada ya umati wa watu kukimbilia katika Kijiji cha Samunge ambacho kipo umbali wa takribani kilomita 400 kutoka Arusha mjini, ili kufika huko ni lazima abiria watumie usafiri wa magari aina ya Toyota Land Cruiser na mabasi. Nauli za magari kuelekea kijijini Samunge zimepanda ghafla na kufikia kiasi cha Sh.
100,000 hadi 130,000 kwa mtu mmoja kwa safari ya kwenda na kurudi wakati nauli ya awali ilikuwa ni Sh. 37,500. Na kwa upande wa magari aina ya Land Cruiser imepaa hadi kufikia Sh. 150,000 na 200,000 kwa mtu mmoja kutoka Sh. 35,000 ya awali.
Kwa upande wa bei za vyakula kijijini hapo imezidi kupaa na kufikia Sh.1,000 kwa sahani hadi Sh. 3,000 kwa sahani, wakati nyama ya mbuzi ya kuchoma ikipanda kutoka Sh. 4,000 kwa mguu hadi Sh. 20,000. Maji ya kunywa yanauzwa kwa Sh. 1,000 hadi Sh. 1,500 kutoka Sh. 500.
Wakizungumzia ongezeko hilo pamoja na Mchungaji Mwasapile akitoa onyo kali kwa watoa huduma hiyo kushusha bei haraka, baadhi ya watu waliokwenda kunywa dawa wanasema wafanyabiashara wamegeuzia gharama za dawa hiyo kwenye mahitaji ya kibinadamu.
“Unajua binadamu tuna matatizo sana mchungaji amepewa huduma hii na Mungu bure na yeye ameamua kutoa bure, lakini imefika kwetu waananchi wanaona hapa ndoyo mahali pa kutajirikia jambo hili si sahihi kabisa.
“Hii yote inatoa taswira kwamba kama ingekuwa si Mungu ndani ya mchungaji na zawadi, akapewa mtu mwingine au ikawa ni geresha kwa watu hakika wangekuwa wanaitoa dawa hii kwa gharama kubwa haijawahi kuonekana,” alisema mgonjwa mmoja.
Hata hivyo baadhi ya watu wengine wameiomba Serikali kuingilia kati kwa kusimamia bei za bidhaa na nauli katika eneo hilo kwani zitazidi kuwaumiza zaidi, ilhali wao wamekwenda kwa ajili ya kupata huduma ya dawa.