Na Ally Daud-MAELEZO
DAWA muhimu za binadamu zinapatikana kwa wingi katika Bohari kuu ya dawa MSD kwa masaa 24 zikiwemo dawa za kutibu Malaria, Kifua kikuu, Ukoma, ARV , dawa za kutuliza maumivu pamoja na Anti- biotic ili kutimiza na kutekeleza sera ya mpango wa Afya wa awamu ya tano. Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es salaam ili kuzungumzia hali ya upatikanaji wa dawa na chanjo nchini.
“Dawa zote muhimu kwa binadamu zinapatikana kwenye bohari kuu ya dawa kwa masaa 24 kinyume na watu na Taasisi zisizo za kiserikali kusambaza maneno kuwa MSD imeishiwa dawa kitendo ambacho sio cha kweli dawa zipo na zinasambazwa kwenye vituo vyote vya afya,” Alisema Mhe. Ummy.
Aidha Ummy amesema kuwa ili kutekeleza mpango wa sera ya afya ya Serikali ya tano ,jumla ya shilingi bilioni 251 zimetengwa ili kuweza kuhakikisha dawa za binadamu zinapatikana kila wakati pindi zinapohitajika kutoka MSD ili kutoa huduma bora kwa watanzania.
Aliongeza kuwa Serikali imetenga Bilioni 85 kwa ajili ya kulipa deni linalodaiwa na MSD ili kuhakikisha Bohari hiyo inajiendesha vizuri na kutokaukiwa dawa pindi zinapohitajika katika vituo vya afya na kutoa huduma za matibabu kwa muda muafaka kwa watanzania.
Mbali na hayo Waziri huyo amesema kuwa tatizo la chanjo kwa sasa limepata ufumbuzi kwani zimeagizwa chanjo za watoto za kifua kikuu dozi milioni 2, chanjo za Pepopunda dozi milioni 1.2 na chanjo za Polio ambazo ni dozi 2 ili kuimarisha hali ya matibabu nchini.
“Tulikuwa na tatizo la chanjo kama wiki nne zilizopita lakini tumejitahidi na tumeweza kuleta chanjo zote muhimu pamoja na kuagiza chanjo za surua ambazo zinatarajiwa kuja hivi karibuni ili kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wingi nchini” alisisitiza Waziri huyo.
Aidha amesisitiza kuwa wanahitaji kununua na kufanya uzalishaji wa dawa katika viwanda vya ndani ili kuweza kuchangia uchumi wa viwanda vya ndani ili tufikie uchumi wa kati.
Waziri Ummy aliwataka Wakurugenzi wa Vituo vya Afya pamoja na Waratibu wa Afya wa Wilaya kuagiza dawa MSD mapema bila ya kusubiri ziishe kabisa kwenye vituo vyao ili kuweza kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.