WAZIRI Mkuu wa Uingereza, David Cameron amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo jana. Chama chake cha Conservative kimepata viti 330 huku kile cha leba kikijipatia 232.
Cameron alisema anapania kuendelea kuiongoza Uingereza kwa umoja. Shirika La BBC lilikisia kuwa Cameron na Chama chake angepata ushindi wa maeneo bunge 329. Chama cha Leba kimepata pigo kubwa huko Scotland kutoka kwa chama cha kitaifa cha Scotland National Party SNP.
Licha ya Matokeo hayo Mazuri huko Scotland ambapo SNP ilisajili ushindi mkubwa wa majimbo 50 chama hicho hakikutamba katika maeneo ya England na Wales. Chama cha The Liberal Democrats wanaelekea kusajili matokeo duni wakiwa tayari wameshinda viti vinane pekee.
Nyota wa chama hicho (Lib Dems) Vince Cable, Ed Davey na Danny Alexander wote wameshindwa katika uchaguzi huo. BBC ilikuwa imebashiri kuwa Conservative watasajili ushindi katika maeneo bunge 329, Labour 233, the Lib Dems 8, SNP 56, Plaid Cymru 3, UKIP2, Greens 1 na vyama vyengine vidogo viti 19.
Hata hivyo kiongozi wa chama cha Leba nchini Uingereza Ed Miliband amesema anajiuzulu kama kiongozi wa chama hicho kufuatia matokeo duni ya Uchaguzi Mkuu. Miliband ambaye amempongeza Waziri mkuu David Cameron kwa kuchaguliwa kwa awamu ya pili amesema kuwa anachukua jukumu la kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi huo.
Chama cha leba kilishindwa vibaya katika uchaguzi huo. Katika hotuba aliyotoa mjini London, Miliband alisema kuwa ni wakati mtu mwengine anafaa kuchukua uongozi wa chama hicho huku akithibitisha kuwa naibu kiongozi wa chama hicho Harriet Harman atashikilia uongozi kwa mda.
-BBC