Na Joachim Mushi
WAFANYABIASHARA wa usafirishaji na wamiliki wa vyombo vya moto jijini Dar es Salaam leo wameendelea kuhaha wakitafuta nishati za mafuta ya dizeli na petroli huku na kule bila mafanikio.
Kero hii ilianza tangu jana baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati za Maji na Mafuta (EWURA) kutangaza kushusha bei bidhaa za mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa.
Maeneo mbalimbali ambayo mtandao huu umeyatembelea umeshuhudia madereva wakizunguka kituo kimoja hadi kingine kutafuta nishati hiyo ambayo imeonekana kuwa lulu sasa tangu kutangazwa kwa mabadiliko ya jana.
Vituo vingi vya mafuta vimeendelea kufungwa huku wahudumu wakidai hawana bidhaa hiyo kwa sasa kwani waliokuwa nayo kwenye vituo yamekwisha.
Thehabari imetembelea maeneo yote ya katikati ya jiji la Dar es Salaam na vituo vingi vilikuwa vimefungwa. Ni kituo cha Oilcom cha makutano ya Barabara ya Morogoro na Mtaa wa Libya ambacho kilikuwa kikitoa huduma. Hata hivyo kero ilikuwa kubwa kwani kilizidiwa na kuamua kutoa mafuta ya elfu 10 tu kwa kila gari ili kila mmoja apate angaliu kidogo. Kituo hicho kilikuwa kikiuza petroli kwa sh. 2004, diseli 1911, hata hivyo mpaka mtandao huu unaondoka kituoni hapo majira ya saa saba mchana petroli ilikuwa imeisha kituoni hapo.
Baadhi ya madereva waliamua kuegesha magari yao sehemu ambazo hawakutarajia na kuanza kuzunguka na vidumu wakitafuta nishati hiyo bila mafanikio.
Thehabari ilitembelea maeneo ya Mwenge, Ubungo, Upanga na pembezoni mwa jiji hakukuwa na vituo ambavyo vilikuwa vikiuza nishati hiyo. Eneo lote la Sinza ni kituo kimoja tu cha Big Bon ambacho kilikuwa kikitoa huduma huku kikiwa na msururu wa magari. Wahudumu walilazimika kutoa mafuta hayo kwa mgawo kama enzi za ulanguzi.
Endapo wauzaji wa vituo hivyo wataendelea na mgomo huo hadi jioni huenda magari mengi yakalazimika kusimamisha huduma kwa kile kukosa nishati hiyo. Akizungumza na mtandao huu Meneja Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo amesema mikutano kati ya wamiliki wa vituo vya mafuta inaendelea mjini Dodoma ili kunusuru hali hiyo. “Tupo kwenye mkutano mazungumzo yanaendelea hivyo sasa siwezi kusema chochote,” alisema Kaguo akizungumza na Thehabari kwa njia ya simu.