Daktari mmoja ahudumia wagonjwa 10,000

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Hussein Mponda

Na Janeth Mushi, Arusha

UPUNGUFU wa watumishi wa afya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha
umesababisha daktari mmoja kuhudumia wagonjwa zaidi ya 10,000
kinyume na viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) vinavyoelekeza daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 7,500.

Hayo yamejulikana kwenye mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Idadi
ya Watu Duniani (DSW) kupitia mradi wa Health Action kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kijamii kwa lengo la kuibua kero anuai kwenye sekta ya afya katika Kata ya Leguruki wilayani Arumeru.

“Tumetoa kilio cha tatizo hili la huduma za afya katika vijiji vyetu
lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kurekebisha mambo ili tupate
huduma ya afya kama watanzania wengine hususan waishio mijini,” alisema
Ndeniengwasinga Joseph kutoka kijiji cha Shishtoni. Alisema kuwa wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakikosa huduma za afya pindi daktari huyo anapokuwa na dharura ya kutokuwepo kazini.

“Imekuwa ni kazi kubwa sana kwa daktari huyu wa hapa katika zahanati yetu ya Nkoasenga, kuhudumia vijiji vitano vyenye watu wengi, ni jambo la muhimu kuletwa kwa daktari mmoja angalau wawe wawili,” alisema Anderson Sikawa Mkazi wa Leguruki.

Aidha Sikawa alieleza kuwa zahanati yao ya Nkoasenga haina majengo ya
kutosha ikiwemo chumba cha kuhifadhi nmaiti na pia haitoi huduma zote
na hivyo itakuwa bora ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya ili
kiweze kutoa huduma za kulaza wagonjwa.

Aliongeza kuwa wananchi wa vijiji hivyo wanalazimika kusafiri zaidi ya
kilomita 60 kufuata huduma za afya katika hospitali ya Wilaya
iliyopo Tengeru jambo ambalo limekuwa likiwagharimu fedha nyingi.

Wakizungumzia masuala ya afya ya uzazi baadhi ya wananchi hao walisema kuwa ufahamu mdogo kuhusu elimu ya afya ya uzazi na kwamba wao wanaishi kwa kufuata mila na desturi katika mambo ya uzazi.

“Mimi kama Mama naelewa umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi na mpango
wa uzazi lakini wakina mama wenzangu hapa kijijini hawafahamu na wala
hakuna uelimishaji wowote unaofanyika kuhusu suala hilo,” anasema
Ndekirwa Sooi.

Alidai kuwa elimu ya uzazi ikitolewa katika jamii wanaume wengi
watabadili mawazo na matendo yao, pia ushiriki wao utaondoa dhana
potofu kuwa elimu ya afya ya uzazi na mpango wa uzazi huwausu
wanawake pekee.

“Kutokana na Wanaume wengi kutopata elimu ya afya ya uzazi kumekuwa
na ongezeko kubw ala watu katika kijiji chetu hivyo elimu hiyo ni
muhimu ikatolewa kusaidia kupunguza kasi ya ongezeko la watu hapa,” alisema Sooi

Meneja utetezi wa DSW- Tanzania, Manka Kway, alisema kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Women in
Development for Science and Technology (WODSTA), Walio katika Mapambano
na AIDs (WAMATA), Evangelical Lutheran Church of Tanzania- Selian (ELCT-Selian).

Wengine ni pamoja na Women and Child Vision (WOCHIVI), Pathfinder
International (PI), Support for International Change (SIC) na Tumaini
Positive (TUPO) chini ya Mradi ujulikanao kama Health Action unaolenga
kuwajengea uwezo mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya utetezi na
ushawishi katika masuala ya afya.