Daktari ‘Feki’ wa Muhimbili Akamatwa..!

Askari akimwongoza mtuhumiwa Mustafa Kitano, anayedaiwa kutoa huduma za utabibu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kinyume na utaratibu, jana.

Askari akimwongoza mtuhumiwa Mustafa Kitano, anayedaiwa kutoa huduma za utabibu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kinyume na utaratibu, jana.


MAOFISA Usalama wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamemkamata mtu anayedaiwa kutoa huduma kwa wagonjwa kinyume cha utaratiba na kwamba, amekuwa akiwatapeli wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu.

Akizungumza ofisini kwake jana, Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminieli Eligaesha alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Mustafa Kitano na kwamba, amekuwa akitumia majina ya Dk Nyirabu na Koba, alikamatwa wakati akimsaidia mgonjwa mmoja.

Eligeisha alisema Februari 22 mwaka huu walipata taarifa kutoka kwa Hussein Haji kuwa, kuna daktari anaitwa Koba alitaka kumtapeli Sh 200,000 ili amtafutie kazi ya udereva kwenye tawi la MNH lililopo Kahama Shinyanga. Inadaiwa Haji alipofika Muhimbili alimpigia simu daktari huyo, lakini aliambiwa kuwa wasingeweza kuonana kwa sababu alikuwa ana kikao na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, badala yake alimtaka akutane na Dk Said Kiliwanga.

“Alimwambia kazi hiyo utakuwa analipwa Sh570,000 na posho kila siku Sh90,000, pia alimwambia amtumie namba yake ya leseni,” alisema Eligaeshi.

Akisimulia jinsi alivyonusurika kutapeliwa, Haji alidai Dk Kiliwanga (ambaye hajakamatwa) alimtaka atume fedha kwenye M-Pesa ili waonane, kitendo alichokataa na kwenda kutoa taarifa kwa walinzi wa hospitali hiyo.

Namna alivyonaswa
Eligaeshi alidai maofisa usalama wa hospitali hiyo walipata taarifa za kuwapo kwa daktari aliyeonekana akiwahudumia wagonjwa na kwenda kumkamata.

Baada ya kutiwa mbaroni, inadaiwa alipekuliwa na kukutwa na kadi tatu za kliniki za wagonjwa wa Muhimbili, kitambulisho cha Peter Daniel mfanyakazi wa hoteli moja Dar es Salaam, vipimo vya kupimia ujauzito, namba nyingi za madaktari wa Muhimbili kwenye simu yake ya mkononi na Sh167,000. Wakati akiwa chini ya ulinzi, mmoja wa wagonjwa wake, aliyefahamika kwa jina la Hassan Madika alimpigia simu na kutakiwa kwenda sehemu aliyokuwa akihojiwa. Mtuhumiwa alikiri kupigiwa simu na Madika.

Kitano ajitetea
Kitano alisema kuwa alifika hospitalini hapo baada ya Madika kumweleza kuwa alikuwa amefanyiwa operesheni wiki iliyopita na kwamba, hawezi kusimama muda mrefu hivyo alikuwa akihitaji msaada wa mtu wa kumpelekea faili sehemu husika.

Haji alipoulizwa na waandishi wa habari, iwapo anamfahamu Kitano alisema alikiri kutomfahamu na kwamba, hajawahi kumwona. Alisema alifika hospitalini hapo kumsaidi Madika na kwamba, tuhuma hizo zinalenga kumchafulia jina hazina ukweli.
Hata hivyo, Kitano alisema yeye siyo tapeli daktari na ameshafanya kazi hospitali mbalimbali za Serikali.

Chanzo: Mwananchi