Moshi
CHAMA cha Walimu (CWT) mkoani Kilimanjaro wamelaani vikali kitendo kilichofanywa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Kalembo cha kuiamuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu kumkamata Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Moshi Vijijini, Hubert Mariki alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kudai haki za wanachama wake.
Katika tamko lao lililotolewa juzi mkoani hapa, baada ya kikao cha Baraza la CWT Mkoa wa Kilimanjaro, chini ya Katibu wa CWT mkoa wa Kilimanjaro, Nathanael Mwandette wamekemea na kulaani kitendo kilichofanywa na Kalembo na kuongeza kuwa kwa sasa baraza hilo halina imani na uongozi wa mkoa kutokana na tukio hilo.
Machi 17 mwaka huu, Kalembo alitoa amri ya kukamatwa kwa Mariki wakati alipokuwa akidai haki za wanachama wake ambao walikuwa wanalidai Shirika la Bima la Taifa Mkoa wa Kilimanjaro fedha zao zaidi ya sh. milioni 300 ambazo ni fedha za michango yao kwa shirika hilo ambazo zimeiva.
Kwa mujibu wa tamko la CWT lililotolewa kwa vyombo vya habari na kusaini na Mwandette, linaeleza kuwa baraza linatafsiri kitendo hicho si tu uzalilishaji, ukandamizaji na ukwamishaji wa upatikanaji wa haki za walimu mkoani Kilimanjaro bali ni kuonesha kutojali haki na maslahi ya walimu kwa ujumla.
Aidha baraza hilo pia limesikitishwa na kitendo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi cha kuwaandikia barua baadhi ya walimu za kuwashusha vyeo walivyopewa hapo awali ambavyo walikuwa wamedumu navyo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Limedai hoja za mkurugenzi huyo kueleza kuwa walimu hao walipewa vyeo hivyo kimakosa hazina msingi kwani ni jambo la kushangaza kuona makosa makubwa kama ya upandishaji vyeo yanafanywa kwa kundi kubwa tena baada ya kudumu kwa takribani mwaka mmoja.
“Mmoja wa walimu hao katika barua aliyoandikiwa na mkurugenzi ya Machi 5 mwaka huu, yenye kumbukumbu Na. MMC/TSD/C.907/134 alikuwa na cheo cha Ofisa Elimu Msaidizi Mwandamizi ngazi ya mshahara ni TGTS E, ameshushwa cheo na kuwa Ofisa Elimu Msaidizi III ngazi ya mshahara TGTS C,” alisema Mwandette katika taarifa hiyo.
Alisema kufuatia matukio yote hayo walimu mkoani Kilimanjaro huenda wakashindwa kutoa mchango wao katika kuboresha taaluma mkoani hapa kwani wanaonekana kana kwamba hawathaminiwi na haki na maslahi yao hupuuzwa hasa kipindi wanapokuwa kwenye harakati za kudai haki zao.
Aliongeza kuwa hali hiyo inatafsiriwa kuwa ni kuvuruga walimu kimaslahi katika kupata mafao ya hitimisho la kazi baada ya kustaafu kwao na pia kuwakatisha tamaa katika jitihada zao za kujielisha ili waweze kufanya kazi zao kiufanisi, hivyo kuitaka Tume ya Utumishi Idara ya Walimu (TSD) kuangalia suala hilo kwa upya ili kutokuwaingiza walimu katika matatizo kutokana na uzembe wa baadhi ya watendaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Bernadette Kinabo alipotakiwa kujibu malalamiko hayo alisema hakuna makosa yoyote yaliyofanyika dhidi ya walimu hao, bali wamepokonywa vyeo walivyopewa kimakosa na mishahara yao itabaki pale pale.