CUF YASISITIZA MAANDAMANO YA CHADEMA NI UCHOCHEZI

Na Mwandishi wetu, Tanga.

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewaasa watanzania kuepuka kushiriki maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa ni ya uchochezi yenye lengo la kuliingiza taifa katika machafuko.

Pia kimeitaka serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutofumbia macho kauli za uchochezi dhidi yake.

Hata hivyo, CUF imesema kinachofanywa na viongozi wa Chadema kwa kuhamasisha wananchi kutoiamini serikali iliyopo madarakani ni uhaini na viongozi wake wanapaswa kukamatwa na kufungwa jela kwa uhaini.

Kauli hiyo ilitolewa katika uwanja wa Tangamano juzi na Mbunge wa Jimbo la Wawi Zanzibar Hamad Rashid.

Alikuwa akimkaribisha Mweyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuwahutubia maelfu ya wakazi wa Tanga kuwashukuru kwa kukipigia kura chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka jana.

Hamad alisema mwaka 1995 Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar iliwakamata na kuwafunga jela miaka mitatu watu 18 akiwamo yeye kama mbunge kwa kutoa kauli ya kuipinga SMZ katika kikao cha Baraza la Wawakilishi .

“Mimi hapa Hamad Rashid mwaka 1995 nilikamatwa na kufungwa jela miaka mitatu na wenzangu 17 kwa kosa la uhaini kwa kutoa kauli za kuipinga serikali i.liyokuwapo madarakani tena ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi ….ila tulikamatwa na kufungwa jela…

‘Ila leo hawa wenzetu Chadema wanapita maeneo mbalimbali ya nchi kuhamasisha maandamano ya kumkataa Rais Kikwete bila serikali kuwashughulikia viongozi hao,” alisema.

Alisema tatizo la vijana wengi wanaoshabikia hali hiyo ni wale wanaofuata mikumbo na baadhi yao kutokuwa na elimu ya kutosha pasipo kutambua kuwa kuipinga serikali iliyopo madarakani ni sawa na uhaini na wanaweza kukamatwa na kufungwa jela.

“Nawaombeni sana wananchi wa mkoa wa Tanga na watanzaia kwa ujumla jiepusheni na maandamano na mikutano inayoandaliwa kwa ajili ya kupinga serikali halali iliyopo madarakani,“ alisema.

Source: New Habari