CSSC Kuadhimisha Miaka 25 ya Huduma kwa Mafanikio Makubwa

CSSC yajivunia hospitali 102 na taasisi 1006 nchi nzima

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC), Peter Maduki.

TUME ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC), inatarajia kuadhimisha miaka ishirini na mitano (25), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992, maadhimisho yatakayofanyika kwa siku mbili tarehe 21 na 22 mwezi Februari katika ukumbi wa Diamond Jubelee na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo, Peter Maduki amesema, maadhimisho hayo yatatumika kutafakari na kuangalia mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta ya afya na Elimu nchini pamoja na kuangalia mchango unaotolewa na taasisi za Mkanisa katika maeneo husika.

“Tunaadhimisha miaka 25 ya kuhudumia jamii kwakuwa sisi ni wadau wakubwa katika kushirikiana na serikali kutoa huduma za jamii, ndiyo maana ukiangalia takwimu, utaona kuwa Makanisa yanamiliki asilimia 14 ya taasisi zote zinazotoa huduma ya afya hapa nchini, wakati huohuo makanisa yanamiliki takribani asilimia 42 ya hospitali zote nchini,” alisema Maduki.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC), Peter Maduki akizungumza na waandishi wa habari. 

“Makanisa bado yanaendelea kuanzisha na kuendesha taasisi za elimu katika ngazi mbalimbali , hadi mwishoni mwa mwaka 2016, Makanisa yalikuwa yanamiliki taasisi zipatazo 1006. Idadi hii ikiwa ni pamoja na vituo vya Elimu ya Awali vilivyosajiliwa serikalini 300, shule za msingi 172, shule za Sekondari 318, Seminari 52, Vyuo vya Ualimu 11, Vituo vya Mafunzo Stadi 126, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki 27,” aliongeza mkurugenzi huyo.

Akizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kwa kipindi chote hicho, mkurugenzi Maduki alisema kuwa Uelewa, Umaskini na Utashi miongoni mwa watendaji na wananchi vimekuwa ni kiwazo kikubwa ambacho hata hivyo alisema wanaendelea kupambana navyo ili kuhakikisha Kanisa linaendelea kutoa huduma zake kwa jamii kwakuwa huo ni wito wake.

Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) inaundwa na Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na ilianzishwa mwaka 1992, kwa dhumuni la kuratibu na kusimamia huduma za kijamii zitolewazo na Taasisi za makanisa hususani za Elimu na Afya Nchini.

Kwa miaka mingi sasa, huduma za jamii zitolewazo na makanisa hususani katika sekta ya Afya na Elimu nchini zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini, huku zikiwa na ubora wa kiwango cha juu unaoonekana katika matokeo ya mitihani mbalimbali kwa upande wa elimu na matibabu bora kwa upande wa afya.