Na Shamimu Nyaki-WHUSM.
Waziri wa Habari Utamaduni,Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye amezindua studio ya redio ya jamii ya ‘Community Media Network of Tanzania’ (COMNET) katika Chuo kikuu Huria( OUT ) itakayotumika kusambaza habari maeneo yenye uhaba wa redio.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam,ambapo Waziri amesema kuwa studio hiyo itasaidia idadi kubwa ya wananchi wanaoishi vijijini kupata habari kutoka Serikalini na kutoa mrejesho wa kile watakachosikia kwa urahisi.
“Ni Studio muhimu kwa ajili ya kusambaza demokrasia kwa watu hasa wale waliopo vijijini kwa vile redio nyingi bado hazijawafikia”Alisema Nape.
Aidha amewataka wanafunzi wa taaluma ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma katika chuo hicho kutumia studio hiyo kujifunza zaidi kwa vitendo na kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari zenye ukweli kutoka vyanzo sahihi ili kutoa ujumbe wenye manufaa kwa jamii.
Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo hicho Prof. Elifas Bisanda amesema studio hiyo imeanzishwa kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni(UNESCO) kwa lengo kutoa elimu kwa jamii ambayo imekuwa haipati habari kwa urahisi.
Amewataka wanahabari na wananchi kwa ujumla kufikisha habari katika studio hizo kwa kuwa inatumia njia ya haraka na rahisi katika kufikisha ujumbe kwa kushirikiana na redio mbalimbali za jamii.
Naye mwakilishi kutoka Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia Elimu,Sayansi,na Utamaduni(UNESCO) Bi. Zulimira Rodrigues amesema studio ya redio ya ‘Community’ ipo kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu maendeleo ya wanawake na vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Mpaka sasa Shirika hilo limefanikiwa kuanzisha redio za jamii katika baadhi ya mikoa ya Tanzania bara ambayo ni Mwanza,Arusha na Tanga na katika baadhi ya maeneo ya Unguja na Pemba.