RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Februari 4, 2014, amepokea hundi ya Sh. milioni 100 kutoka Benki ya CRDB kusaidia wahanga wa mafuriko yaliyozikumba wilaya tatu za Kilosa, Mvomero na Gairo katika Mkoa wa Morogoro, mwezi uliopita.
Rais Kikwete amekabidhiwa hundi hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa pia na William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia pia masuala ya maafa.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi hiyo kwa Rais Kikwete, Dk. Kimei amesema kuwa fedha hizo ni sehemu ya Sh. Milioni 850 ambayo ni asilimia moja ya faida ya Benki hiyo ambayo hutengwa kila mwaka kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za jamii.
“Sote tumeona madhara makubwa yaliyosababishwa na mafuriko haya. Watu wengine wamepata hasara – akinamama, watoto, wajawazito na wazee. Hawa wote wanahitaji misaada ya ziada ili kukabiliana na athari za mafuriko hayo,” amesema Dk. Kimei.
Akizungumza kabla ya kupokea hundi hiyo, Rais Kikwete ameelezea kwa ufupi mafuriko hayo yaliyotokea alfajiri ya Januari 22, mwaka huu, 2014 na athari ambazo zimetokana na mafuriko hiyo katika maeneo ya Magole, Dakawa na Mateteni huko Dumila, Wilaya ya Mvomero, ambayo aliyatembelea mwishoni mwa mwezi uliopita kujionea madhara.
“Waswahili husema kuwa ajali haina kinga na ni kweli. Unajua mafuriko yaliyotokea katika eneo la Dumila hayakutokana na wala na mvua ya pale. Mvua ilinyesha kule Kiteto, Mkoa wa Manyara, lakini walioathirika kwa mafuriko ni hawa jamaa zetu wa Dumila. Bahati tu ni kwamba mafuriko hayo yalilikumba eneo hilo alfajiri wakati watu tayari wameamka na ndio maana hakuna mtu aliyepoteza maisha yake katika eneo hilo,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Watu wamepata hasara kubwa. Baadhi nyumba zao zimesombwa na kuzolewa na maji, nyingine zimebomoka, watu wamepoteza mali zao nyingi kama vile nguo na wengine hata chakula chao kimesombwa na maji. Wanahitaji msaada na kwa kweli sisi katika Serikali tunaishukuru sana CRDB kwa kutoa msaada huu kwa sabababu unachangia katika jitihada za Serikali kukabiliana na tatizo hili.”
Akizungumza katika shughuli hiyo, Mheshimiwa Lukuvi amesema kuwa tathmini mpya imeonyesha kuwa watu walioathirika katika mafuriko hayo ni 9,268 na kati ya watu hao kaya 522 hazina makazi kabisa baada ya nyumba zao kubomolewa na maji, nyingi zaidi 466, zikiwa katika Wilaya ya Kilosa.
Amesema kuwa nyumba 537 zimeharibika hata kama wenye nyumba hizo bado wanaendelea kuishi ndani ya nyumba hizo na nyingine 1,036 ziliingiwa na maji hata kama hazikuharibika.