Na Nicodemus Ikonko, EANA, Arusha
MOJA ya taasisi za fedha zenye mafanikio nchini Tanzania, Benki ya CRDB, itafungua tawi lake mjini Bujumbura, Burundi, kabla ya mwisho wa mwaka huu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa benki hiyo kuvuka mipaka ya nchi yake.
Meneja Mkuu wa Benki ya CRDB Burundi, Bruce Mwile alilithibitishia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kwa njia ya simu Jumanne juu ya uvumi unaoendelea kutanda katika tasisi za fedha hapa nchini kuhusu hatua hiyo.
“Tawi moja litafunguliwa mjini Bujumbura mwaka huu lakini siweze kukueleza kwa uhakika kuwa ni lini kwa vile yapo masuala kadhaa yanayohitaji kukamilishwa kwanza,” alifafanua Bruce.
Alisema kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi, hivi sasa inajenga ofisi kuu katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, ambayo ndiyo itakuwa kitovo cha kuzalisha matawi mengine ya benki hiyo katika nchi yenye kutegemea uchumi wake kwa kuuza nje chai na kahawa.
“Hivi sasa tunajenga makao makuu hapa (Bujumbura) na tutakuwa na matawi mengine zaidi ndani ya jiji,” alisema huku akijizuia kutoa taarifa zaidi hadi siku ya uzinduzi rasmi. Burundi ni moja ya nchi wanachama inayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mpya. Wanachama wengine ni Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda.
Tayari nchi hizo zimeshafikia hatua mbili za kuelekea kwenye mtangamano ikiwa ni pamoja na Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja na wanampango wa kuingia katika hatua ya tatu ya Umoja wa Fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa Juni, mwaka huu mjini Arusha, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei alisema kampuni tanzu ya benki hiyo nchini Burundi, ingefunguliwa rasmi mwezi uliopita lakini imecheleweshwa kutoka na kile alichokiita “matatizo ya kilojistiki”.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa International Business and Management Consultant Ltd ya mjini Arusha, Simon Mapolu ameipongeza hatua hiyo kwa kusema, “Benki ya CRDB imetafsiri kwa vitendo dhana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuzitaka nchi wananchama kufanya biashara nje ya mipaka yake.”
Alifafanua zaidi kwamba hatua hiyo itatoa msukumo kwa “Kampuni za kitanzania kupata uzoefu wa kufanya biashara kimataifa kwa uweledi na ufanisi katika soko la dunia.”
Kwa mujibu wa Mapolu hatua hiyo ya CRDB, itaongeza faida na gawio kwa wanahisa wake, sambamba na pato la taifa kwa kulipa kodi zaidi. Benki ya CRDB itakuwa ni ya pili ya kitanzania kufungua tawi nje ya mipaka ya nchi yake ikitanguliwa na benki ya Exim yenye tawi katika visiwa vya Comoro.
Ni Kenya peke yake kati ya nchi tano wanachama wa EAC ndiyo yenye matawi ya benki ya Kenya Commercial Bank katika nchi zote.