Congo Brazzaville Yawasili Kuikabili Serengeti Boys

Baadhi ya wachezaji wa Serengeti Boys

CONGO Brazzaville imewasili leo alfajiri (Novemba 15 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya raundi ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Tanzania (Serengeti Boys) itakayochezwa Jumapili.

Timu hiyo imewasili kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 30 wakiwemo wachezaji 18 ambapo imefikia kwenye hoteli ya Sapphire. Mechi hiyo itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Serengeti Boys inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa chini ya Kocha wake Jackob Michelsen wakati Congo inafanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Karume, na kesho (Novemba 16 mwaka huu) asubuhi na jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja huo huo.

Timu hiyo ambayo katika raundi ya pili iliitoa Zimbabwe itafanya mazoezi yake ya mwisho Jumamosi jioni kwenye Uwanja wa Taifa. Viingilio kwenye mechi hiyo ni sh. 10,000 kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP C ni sh. 2,000 tu. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu ni sh. 1,000 tu.

Makocha wa timu zote mbili na manahodha wao watakutana na waandishi wa habari Jumamosi saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuzungumzia maandalizi yao kwa ajili ya mechi hiyo kabambe.