Clouds FM Yakanusha Kutumika Kisiasa na CCM

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Joseph Kusaga

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Joseph Kusaga


Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Clouds Media Group wamiliki wa redio Clouds FM, Choice FM na Clouds Televisheni wamepinga vikali juu ya tuhuma kwamba wanatumiwa kisiasa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza leo kwa njia ya simu kutokea nchi za Falme ya Kiarabu, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Joseph Kusaga alisema chombo hicho cha habari hakitumiki kukibeba chama chochote na kipo tayari kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote bila kubagua.

Alisema tuhuma za kwamba chombo hicho kinatumiwa na CCM hazina msingi wowote zaidi ya uzushi na huenda watu wanaoeneza maneno hayo wanatumwa kukidhohofisha chombo hicho kibiashara jambo ambalo alidai haliwezi kufanikiwa.

Aidha akizungumziwa tuhuma za kwamba kampuni hiyo inataka kuuzwa kwa Rostam Aziz alisema ni za uzushi wala uongozi wake haujafikiria kufanya hivyo kwa kuwa bado wanafanya vizuri kibiashara huku wakiwa na malengo mengi ya kufanya.

Alisema Clouds FM imepanga kujitanua nchi nzima ili kusikika mikoa yote mipango ambayo inaendelea vizuri hatua kwa hatua huku viongozi wakishirikiana vizuri na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Jana kupitia mitandao ya jamii ilitoka taarifa ambayo ilisambaa kwa kasi maeneo mbalimbali ikieleza tayari kampuni hiyo imeuzwa na kinachofanyika ni kuwasainisha wafanyakazi wake mikataba mipya kutoka kwa aliyeinunua.